Mtetezi wa haki za Wafalastina ashtumu utekaji nyara wa wanamaji wa Israel dhidi ya meli ya wahisani wa kimataifa

Mtetezi wa haki za Wafalastina ashtumu utekaji nyara wa wanamaji wa Israel dhidi ya meli ya wahisani wa kimataifa

Richard Falk, Mkariri/Mtaalamu Maalumu wa UM juu ya haki za binadamu kwenye maeneo ya WaFalastina, yaliokaliwa kimabavu na Israel tangu 1967, amelaumu utekaji nyara, haramu, ulioendelezwa wiki hii na manowari za Israel, kwenye bahari kuu, dhidi ya ile meli ndogo ya wanaharakati wa amani, iliokuwa imechukua shehena ya madawa na vifaa vya ujenzi kwa umma wa Tarafa ya Ghaza.

Hivi sasa umma wa Ghaza unakabiliwa na vikwazo kadha wa kadha. Kwa mujibu wa mtaalamu wa haki za binadamu "kitendo cha Israel kinadhihirisha utekelezaji wake wa vikwazo katili dhidi ya umma mzima wa WaFalastina wa Ghaza, hatua ambayo inaharamisha Kifungu cha 33 cha Mkataba wa Nne wa Geneva, unaopiga marufuku vitendo vyote vya kuadhibu, kwa pamoja, ule umma uliokaliwa kimabavu na utawala wa nje." Wanaharakati wa amani 21 waliokuwa ndani ya meli ndogo ilioshikwa na Israel walikamatwa na sasa hivi wapo kizuizini kwa madai ya "kuingia nchini bila ruhusa", licha ya kuwa hawakuwa na azma ya kwenda Israel wakati meli yao ilipotekwa nyara kwenye bahari kuu, mbali na Israel wakati ikielekea Tarafa ya Ghaza kutokea Cyprus. Miongoni mwa watu walioshikwa na Israel kutoka meli hiyo alikuwemo mshindi wa Tunzo ya Amani ya Nobel wa kutoka Jamhuri ya Ireland, Mairead Maguire, na vile vile mbunge wa zamani wa Marekani, ambaye pia aliwahi kuwa mgombea uraisi wa taifa lake, Cynthia McKinney.