Hapa na pale

2 Julai 2009

KM Ban Ki-moon ambaye yupo Ujapani kwa hivi sasa, Ijumatano alikutana kwa mazungumzo na viongozi wa taifa hilo, ikijumlisha Waziri Mkuu Taro Aso, na walisailia mwelekeo wa kufuatwa na jumuiya ya kimataifa ili "kukamilisha makubaliano yanayoridhisha" kwenye mkutano ujao wa Copenhagen juu ya udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Vile vile walishauriana juu ya masuala yanayoambatana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK), Myanmar, mchango wa Ujapani katika kuendesha shughuli mbalimbali za UM, hasa katika operesheni za kulinda amani, na pia kuzungumzia taratibu za kufuatwa na wafanya biashara zitakazohakikisha kunakuwepo maendeleo yanayosarifika. Alkhamisi KM ataelekea Singapore kabla ya kwenda Myanmar Ijumaa.

 Shirika la UM la Usaidizi Amani Iraq (UNAMI) limelaani, kwa kauli kali, shambulio maututi la bomu lilioripuliwa kwenye marikiti ya al-Shourga katika jimbo la Kirkuk, hii leo, kitendo ambacho kilisababisha darzeni za vifo na majeruhi kadha ya watu wasio hatia. UM unaamini tukio hili limekusudiwa kuchochea uhasama wa kimadhehebu na mapigano ya kikabila miongoni mwa raia wa Iraq. UNAMI imewatumia mkono wa pole aila zote zilizofiwa na kuwaombea majeruhi wapone haraka, na vile vile kuyataka makundi yote ya kiraia nchini "kutoitika pendekezo la uchokozi wa tukio hilo na kujiepusha na ari ya kutaka kulipa kisasi."

Tume Maalumu ya Uchunguzi, iliodhamaniwa jukumu la kutafuta ukweli na mazingira yaliosababisha mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, Benazir Bhutto imeanzisha rasmi shughuli zake siku ya leo, tarehe 01 Julai (2009), huduma ambazo zitaendelezwa katika miezi sita ijayo. Tume hii ya wajumbe watatu, inaongozwa na Balozi Heraldo Muńoz wa Chile na kujumuisha vile vile Marzuki Darusman wa Indonesia na Peter Fitzgerald wa Jamhuri ya Ireland. Tume inatazamiwa kuzuru Pakistan mnamo siku za karibuni, kwa mara ya kwanza, kwenye tarehe ambayo bado haijatangazwa.

Christopher Ross, Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Sahara ya Magharibi amefanikiwa kumaliza ziara ya pili kwenye jimbo la mgogoro, tangu alipoanza kazi mwanzo wa mwaka. Ijumanne alikuwepo Madrid, kwenye mguu wa mwisho wa ziara ya wiki moja ya eneo, na alionana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uspeni, taifa liliotawala Sahara Magharibi miaka ya nyuma. Kabla ya hapo Ross alizuru Algiers, Tindouf, Nouakchott na Rabat, na alinakiliwa akisema ana matumaini ya kutia moyo, kuhusu mkutano ujao, usio rasmi, utakaowakilisha duru ya tano ya majadiliano yanayaotazamiwa kuleta suluhu ya kuridhisha kuhusu mgogoro wa Sahara ya Magharibi, mzozo ambao umeselelea kwa muda mrefu, na umekwamisha zile juhudi za kukamilisha mamzungumzo ya kuleta muungano miongoni mwa mataifa ya Afrika kaskazini-magharaibi (Maghreb).

Shirika la Ulinzi Amani la UM kwa JKK (MONUC) limetangaza taarifa ilioshtumu majaribio ya wafungwa ya kutoroka tena kwenye Gereza Kuu la Aru, liliopo jimbo la kaskazini-mashariki la Ituri, yaliofanyika Ijumaa iliopita, ikiwa na mara ya pili katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja. MONUC ilikiri kwamba hali katika gereza la Aru ni mbaya na hailingani na vigezo vya kimataifa, mazingira ambayo taarifa ya MONUC ilisisitiza imepamba takriban katika magereza yote ya taifa. Serikali ya JKK imenasihiwa kujitahidi kusawazisha hali hii na kuimarisha usalama katika vituo vyote vya kufungia watu viliopo nchini. Wakati huo huo MONUC imetangaza ya kuwa kuanzia Januari 2009 raia wa Rwanda 10,000 na waasi wa zamani walifanikiwa kurejeshwa makwao kwa khiyari kutokea JKK.

Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID), yaani Jenerali Martin Luther Agwai, anaendelea na ziara zake za kutembelea kambi za wanajeshi waliopo chini ya uongozi wake katika Darfur. Ijumatano Jenerali Agwai alitembelea Batalioni ya Wamisri waliopo katika sehemu ya Ed Al Fursan, Darfur Kusini. Kadhalika, Naibu Kamanda Mkuu wa UNAMID, Jenerali Duma Dumisani naye pia amezuru miji ya Darfur Kusini ya Nyala, El Daein na Muhajeriya. Wakati huo huo, Idara ya Masuala ya Kiraia ya UNAMID ilifanyisha warsha maalumu wa siku moja kuzingatia ujenzi wa jamii ya amani katika eneo la Nyala, ambapo kulijadiliwa taratibu zinazohitajika kutatua mizozo inayohusu umilikaji wa ardhi, mfumo wa sheria ya mpito na njia ya kutumiwa kuzuia migongano baina ya wafugaji na wakulima. Warsha huu uliwakusanyisha jumuiya za kiraia, maofisa wa Serikali na wadau wengine wa kutoka Chuo Kikuu cha Nyala.

Mapema Ijumatano Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro alihutubia kikao cha kawaida cha 13 cha Baraza la Umoja wa Afrika, kwa niaba ya KM, kilichojumuika kwenye mji wa Sirte, Libya. Alisema kwenye risala yake jitihadi za kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) katika Afrika haziridhishi, na hazina uwiano na kaulimbiu ya mkutano, ambayo ilitilia mkazo umuhimu wa kukuza kilimo kuimarisha uchumi barani humo. Alihadharisha maisha ya mamilioni ya wakazi wa Afrika sasa hivi yanahatarishwa na matatizo ya mabadiliko ya hali ya hewa, mizozo inayotumia nguvu na mifumko ya mabadiliko ya serikali yasiolingana na katiba, masuala ambayo ni lazima kudhibitiwa na nchi husika haraka. Aliwahimiza viongozi wakuu wa kimataifa na wajumbe wa mkutano kujitahidi kuandaa hatua imara zitakazohakikisha raia masikini na walio dhaifu watapata hifadhi inayofaa na kuhakikisha idadi yao haitopanuka zaidi.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) imeripoti wafungwa tisa wa taasisi hiyo wamehamishwa kwenye mji wa Cotonou, katika Jamhuri ya Benin kutoka Kituo cha Kufungia Watu cha UM kilichopo Arusha, Tanzania. Uhamisho huu unafungamana na maafikiano ya mwezi Mei baina ya Raisi wa Mahakama ya ICTRna Serikali ya Benin. Wafungwa hawa tisa inasemekana wameshaanza kuutumia muda uliosalia wa kifungo chao kwenye gereza ya Benini iliopo mji wa Port-Novo.

Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) na Benki Kuu ya Dunia wamewasilisha taarifa ya pamoja iliobainisha wasiwasi wao kuhusu upungufu wa misaada ya kimataifa kuhudumia miradi ya uzazi bora, kwa kisingizio cha kupamba mzozo wa uchumi wa dunia, mwelekeo ambao mashirika haya yanaamini unakwamisha jitihadi muhimu za kutekeleza kwa wakati yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayohusu afya bora kwa mama wajawazito. UNFPA inakadiria wanawake 500,000 hufariki kila mwaka katika wakati wa kuzaa au kwenye kipindi wanapochukua mimba, kwa sababu ya matatizo ya afya wanayokabiliwa nayo, matatizo ambayo yanazuilika na rahisi kutibiwa. Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA, Thoraya Ahmed Obaid alionya kwamba tusidhani "maendeleo ya kuhudumia uzazi bora hurejeshwa nyuma kwa sababu ya ukosefu wa maarifa, bali anaamini huduma hizi zinazorotishwa kihakika kwa sababu ya kukabwa kimaendeleo na ukosefu wa nia thabiti za kisiasa zinazotakikana kutunza haki halali za wanawake na kuhifadhi afya yao, kwa ujumla."

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter