Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe Maalumu wa Maziwa Makuu hakuridhika na maendeleo ya kurudisha amani

Mjumbe Maalumu wa Maziwa Makuu hakuridhika na maendeleo ya kurudisha amani

Mjumbe Maalumu wa UM juu ya Masuala ya Maziwa Makuu, Olusegun Obasanjoaliyekuwa raisi wa zamani wa Nigeria, ambaye anazuru Mako Makuu kushauriana na wakuu wa UM kuhusu hali ya eneo, aliwaambia waandishi habari Ijumanne kwamba maendeleo ya kurudisha utulivu na amani katika eneo la vurugu, la mashariki katika JKK yanajikokota, hasa kwenye zile juhudi za kukomesha uhasama baina ya makundi ya waasi na vikosi vya Serikali.

 Alisema utekelezaji wa maafikiano yaliotiwa sahihi tarehe 23 Machi (2009) na Serikali pamoja na kundi la waasi la CNDP (Congress for People's Defence), ulibainisha mafanikio haba aliyoyatafsiri kama "furushi la mchanganyiko". Alieleza kwamba sheria ya msamaha wa makosa ya kisiasa na makosa ya kiserikali imesajiliwa rasmi na kusababisha baadhi ya wafungwa kuachishwa. Kadhalika, lile kundi la waasi wa zamani la CNDP sasa limegeuzwa kuwa chama cha kisiasa, aliongeza kusema Obasanjo. Kuhusu operesheni bia za kijeshi baina ya vikosi vya JKK na Rwanda dhidi ya kundi jengine la waasi la FDLR (Democratic Liberation Forces of Rwanda), Obasanjo alithibitisha juhudi hizi zilifanikiwa kurudisha hali ya kuaminiana na kuimarisha uhusiano bora, na ulio mzuri baina ya mataifa hayo jirani.