Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA imeripoti 170,000 wahajiri Mogadishu kufuatia mfumko mpya wa mapigano

OCHA imeripoti 170,000 wahajiri Mogadishu kufuatia mfumko mpya wa mapigano

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mapigano yalifumka tena katika wilaya za Mogadishu za Karaan na Hodan mnamo mwisho wa wiki iliopita.

Kwa mujibu wa taarifa za OCHA, tangu uhasama huo kuanza katika  tarehe 07 Mei hadi Ijumatatu ya tarehe 29 Juni (2009), watu 170,000 waliripotiwa kuuhajiri mji wa Mogadishu na kuelekea kwenye sehemu nyengine za nchi kutafuta hifadhi. Lakini licha ya mazingira haya ya mapigano, bandari ya Mogadishu imeripotiwa inaendelea bado kufanya kazi, na misaada ya kiutu inayopitishiwa bandarini humo, inapelekewa umma muhitaji na mashirika ya kimataifa, kwenye sehemu mbalimbali za nchi. Ripoti ilisema mnamo tarehe 27 Juni, tani 13,600 za chakula ziliwasili salama Mogadishu, kutokea Mombasa, Kenya kwenye meli zilizokuwa zikiongozwa na manowari za Umoja wa Ulaya (EU). Kadhalika, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) na washirika wenzi wamejumuika kwa sasa kuhudumia maji safi watu 200,000, kwa kupitia ushoroba wa Afgooye. Vile vile OCHA imeripoti ukame unahatarisha maisha ya watu 700,000 nchini Usomali, wanaojumuisha wafugaji na aila kadha zenye kuishi katika mji mkuu, umma ambao hutegemea mapato na chakula kutoka biashara ya wanyama wa mifugo.