Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM anatarajiwa kuzuru rasmi Myanmar kuanzia tarehe 03 - 04 Julai, kwa kuitika ombi la Serikali. Atakapokuwepo huko atakutana, kwa mashauriano ya ana kwa ana, na viongozi wakuu wa Serikali ambapo wanatarajiwa kuzungumzia masuala kadha yenye umuhimu kwa UM na jamii ya kimataifa. Alitilia mkazo kwenye mazungumzo yao mambo matatu yatapewa umuhimu wa hadhi ya juu, kwa kulingana na hali ya kisiasa ilivyo nchini kwa hivi sasa. Masuala hayo yanahusu, awali, kuachiwa wafungwa wote wa kisiasa, ikijumlisha Daw Aung Suu Kyi; kurudisha mazungumzo ya upatanishi kati ya Serikali na Wapinzani; na kusailia maandalizi ya uchaguzi wa taifa ulio huru na wa haki.

KM ameripoti kulaani, kwa kauli nzito kabisa, mashambulio na mauaji yaliotukia majuzi katika miji ya Baghdad, Kirkuk na jimbo la Anbar nchini Iraq ambapo idadi kubwa ya watu waliripotiwa kuuawa na kujeruhiwa. Alielezea kuwa yupo pamoja na Serikali na umma wa Iraq dhidi ya vitendo vyote vya kutumia mabavu dhidi ya raia. Alikumbusha Iraq ilielekea kwenye mkondo wa kurudisha tena utulivu na amani nchini katika miezi ya karibuni. Aliusihi umma wa Iraq kuendelea kupinga vile vitendo vilivyodhamiria kuchochea na kupalilia vurugu ziada ndani ya nchi.

Tume ya Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu iliodhaminiwa jukumu la kutafuta ukweli juu ya mashambulio ya vikosi vya Israel katika Tarafa ya Ghaza, inayoongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, leo imekamilisha duru ya kwanza ya kusikiliza, kwa siku mbili, ushahidi unaosikitisha na kutisha uliotolewa na waathirika wa mashambulio ya Israel, na vile vile kusikiliza hoja za wataalamu na watu wengine walioshuhudia maafa yaliotukia wakati wa mapigano. Jaji Goldstone aliwaambia waliotoa ushahidi, waliokusanyika kwenye Mji wa Ghaza, ya kuwa yeye kama "binadamu mwenziwao" akijumuika na wajumbe wa tume, hisia zao zilizirai na waliyoyasikia na watazisajili hisia hizo kwenye kumbukumbu juu ya namna walivyohuzunishwa na maumivu na mateso walioshuhudia wakazi wa Tarafa ya Ghaza miezi ya nyuma.

Baraza la Usalama asubuhi lilifanyisha mkutano wa hadhara kusailia operesheni za ulinzi amani za UM. Manaibu KM juu ya Masuala ya Ulinzi Amani, Alain Le Roy pamoja na Susana Malcorra walielezea mabadiliko na mageuzi yanayohitajika kufanyika katika kipindi cha sasa ili kuendesha shughuli zao kwa mafanikio. Le Roy aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa sasa, ambapo kuna michango haba ya fedha za kuendesha shughuli za Idara ya UM juu ya Operesheni za Kulinda Amani Ulimwenguni (DPKO), jumuiya ya kimataifa itawajibika kufanya marekibisho yanayolingana na uwezo uliopo. Alitahadharisha kwamba muongezeko wa gharama za kuendesha shughuli za ulinzi amani, pamoja na matakwa ya kuongeza idadi za wanajeshi na uwezo unaohitajika kuhudumia operesehni za amani ni mambo yanayolazimika kudhibitiwa haraka, kwa sababu hali hiyo haiwezi kuruhusiwa kuendelea kupanuka bila kikomo wakati uwezo wa kuyatekeleza majukumu yote hayo haupo.

Jenerali Martin Luther Agwai, Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) mwisho wa wiki iliopita alizuru wanajeshi waliosambazwa kwenye kambi za Graida na Marla, katika Darfur Kusini. Alijadiliana nao masuala yanayohusu operesheni za UNAMID na mahitaji yao ya kila siku. Wakati huo huo, maofisa wengine wa UNAMID walizuru eneo la Kutum, katika Darfur Kaskazini kuthibitisha ripoti za kurejea wahamiaji vijijini, kwa khiyari, na kutathminia mahitaji yao. Wanakijiji waliiarifu UNAMID kwamba aila 2,300 zilisharejea makwao na sasa wanahitajia kufadhiliwa kidharura misaada ya kunusuru maisha. Mashirika ya UM juu ya miradi ya chakula, WFP na huduma za watoto, UNICEF sasa hivi yanajaribu kuwasaidia wanakijiji kupata chakula na misaada mengine ya kiutu. Maofisa wa UNAMID vile vile walizuru miji ya Masri na El Manara kuendeleza tathmini ya mahitaji ya wakazi wa huko, halkadhalika.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR) imeripoti mawakili wa utetezi na wale wanaoendesha mashtaka wamemaliza kutoa hoja zao kwenye ile kesi inayowahusu maofisa wanne wa jeshi la zamani la Rwanda, ambao walituhumiwa kushiriki kwenye mauaji ya halaiki na makosa ya jinai dhidi ya utu. Watuhumiwa hawa wanajumlisha pia Jenerali Augustin Bizimungu, aliyekuwa afisa mnadhimu mkuu wa jeshi la Rwanda, pamoja na Jenerali Augustine Ndindiliyimana, aliyekuwa vile vile afisa mnadhimu wa Vikosi vya Ulinzi vya Gendamarie. Mwendesha mashitaka amependekeza watuhumiwa wapewe adhabu ya kifungo cha maisha. Kwa mujibu wa taarifa za UM kesi ilichukua siku 392, ambapo Mahakama ilisikiliza ushahidi wa kiapo uliotolewa na watu 208. Mahakama ya ICTR bado haijatangaza siku ya kutoa hukumu.

NKM Asha-Rose Migiro ameondoka New York magharibi ya leo akielekea Sirte, Libya kuhudhuria, kwa niaba ya KM, Kikao cha Kawaida cha 13 cha Baraza la Umoja wa Afrika kitakachokutana kuanzia tarehe 01 - 03 Julai (2009). NKM anatazamiwa kuhutubia kikao chenye kaulimbiu isemayo "Tuwekeze Kilimo ili Kukuza Uchumi na Akiba ya Chakula Afrika."

Baraza Kuu la UM katika mwezi Disemba mwaka jana, lilipitisha mwito wa kupiga marufuku kabisa uvutaji sigara ndani ya majengo ya UM. KM amechukua hatua kadha kuhakikisha amri hiyo inatekelezwa na kila mtu katika Makao Makuu, ikijumlisha uwekaji wa alama za "Hakuna Ruhusa Kuvuta Sigara" zilizotundikwa kwenye kila mlango wa kuingilia Makao Makuu. KM alisema sehemu maalumu iliwekwa kando, nje ya majengo ya UM, ambapo wafanyakazi wa UM wataruhusiwa kuvuta sigireti. Kadhalika, maduka yaliomo ndani ya majengo ya Makao Makuu hivi sasa hayaruhusiwi tena kuuza sigara, kama ilivyopendekezwa na mwito wa Baraza Kuu.