Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bodi la Utawala UNCTAD kutathminia ufufuaji wa kilimo Afrika

Bodi la Utawala UNCTAD kutathminia ufufuaji wa kilimo Afrika

Bodi la Utawala la Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) linatarajiwa Ijumanne jioni kukutana Geneva, kufanya tathmini kuhusu juhudi za kufufua kilimo katika bara la Afrika, huduma ambazo zimezorota katikati ya kipindi kilichopambwa na athari haribifu zilizoletwa na mizozo ya uchumi dhaifu kwenye soko la kimataifa.

 Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa wataalamu wa uchumi wa Shirika la UNCTAD watu milioni 300 katika Afrika, yaani sawa na thuluthi moja ya idadi ya watu wa bara hilo, hukabiliwa kila siku na njaa sugu. UNCTAD ilikiri kwamba bei za chakula kwenye mazingira ya mizozo ya chakula duniani zilionyesha dalili ya kuteremka, tukilinganisha na bei za wakati wa kiangazi katika 2008, ambapo mavuno ya bidhaa za chakula yalistawi sana na bei zilikuwa za juu. Lakini licha ya mteremko huo, ilisisitiza UNCTAD, kiwango cha bei za chakula kwa sasa katika Afrika bado ni cha juu sana na watu wa kawaida hawakimudu. Kadhalika, UNCTAD ilibainisha uzalishaji wa chakula katika Afrika ni kadhia iliopitwa na muongezeko mkubwa wa idadi ya watu, na imeelemewa na matatizo ya kuenea kwa kasi kwa wakazi wa katika miji na vile vile ulaji tofauti wa umma wa kawaida. Mataifa ya Afrika, ilinasihi UNCTAD, yanahitajia misaada maridhawa, ya dharura, kutoka wahisani wa kimataifa itakayoleta marekibishio mapya kwenye kilimo, kwa kuzalisha mavuno yanayowiana na mahitaji ya umma, hali ambayo inatarajiwa kusaidia kupunguza shida za njaa, kwa ujumla, barani humo.