Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM alikutana na viongozi wa kundi la Wapatanishi wa Pande Nne juu ya Mashariki ya Kati kwenye mji wa Trieste, Utaliana na walizingatia masuala matano muhimu: mwelekeo unaofaa kuchukuliwa kufufua majadiliano ya amani kati ya Israel na Falastina; kuwasaidia wenye mamlaka wa KiFalastina (PA) kutawala bora kwenye maeneo yao na kukuza uchumi; hali katika Tarafa ya Ghaza; suala la kuleta amani kamili kati ya Israel na Syria, na Israel na Lebanon; na kusailia Mkutano Mkuu wa Moscow utakaofanyika baadaye kutathminia uwezekano wa kurudisha amani katika Mashariki ya Kati.

Wiki moja baada ya kufanyika majaribio ya kutoroka jela katika JKK, ambapo wanawake wafungwa kadha walinajisiwa kimabavu na walinzi wa magereza Shirika la UM juu ya Shughuli za Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) lililazimika kuzingatia taratibu mpya za utawala wa katika magereza, kwa ushirikiano na Wizara ya Sheria nchini. MONUC ikishirikiana na Wizara ya Sheria wataendeleza mafunzo ya siku 10 mjini Kinshasa, mpaka tarehe 03 Julai (2009), kwa maofisa 50 watakaowakilisha vyuo vikuu, mahakama, jumuiya za kiraia na utawala wa magereza.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ametoa risala maalumu leo hii kuihishimu Siku ya Kimataifa juu ya Ushikamano na Waathirika wa Mateso, taarifa iliokuwa na mwito uliowahimiza viongozi wa dunia kutoa ilani, ilio wazi, na isio na mashaka itakayosisitiza vitendo vya mateso havitovumiliwa abadan na jumuiya kimataifa. Pillay aliyakaribisha maamuzi ya Raisi wa Marekani kufunga magereza ya Guantanamo, na kupiga marufuku vitendo vyote vya kutesa watu, hususan yale mateso ya kumwagia mtuhumiwa maji kwa tishio la kumzamisha. Lakini Pillay alisema juu ya maamuzi hayo angelipendelea sana kuona hatua nyengine zinachukuliwa na Serikali ya Marekani kabla magereza ya Guantanamo kufungwa, zitakazohakisiha wale wafungwa waliosalia kwenye jela hizo ama wanafikishwa mahakamani - kama wanavyofanyiwa watuhumiwa wengineo kujua kama ni wakosa au la - na kama hakuna ushahidi dhidi yao waachiwe.

Mkutano Mkuu wa UM Kuhusu Mzozo wa Uchumi Duniani na Athari Dhidi ya Maendeleo ulihitimisha kikao cha siku tatu Ijumaa, ambapo Mataifa Wanachama yalipitisha waraka wa maafikiano ya pamoja, yaliyowakilisha hatua ya awali ya mradi wa muda mrefu, wenye makusudio ya kuelekeza ulimwengu kwenye mwelekeo mpya wa ushikamano wa pamoja katika usuluhisha wa matatizo ya uchumi wa kimataifa, ushikimano utakaofarajia pia utulivu unaosarifika kwenye soko la kimataifa, kwa kulingana na taarifa ya Raisi wa Baraza Kuu, Miguel d'Escoto. Alinakiliwa akisema Baraza Kuu - ambalo alilitafsiri kama Kundi la "G-192" - limefanikiwa kuanzisha rasmi jukwaa muhimu, la kutumiwa na Mataifa Wanachama kushauriana kipamoja juu ya masuala yanayohusu uchumi na fedha katika dunia. Aliongeza kwa kusema Baraza Kuu linatarajiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi husika, kwa kupitia tume maalumu ya utendaji, itakayozingatia mada kadha, mathalan, udhibiti wa mizozo, marekibisho kwenye usanifu wa mifumo ya uchumi na fedha ulimwenguni, taratibu za kuhudumia madeni ya nchi za kigeni na utulivu katika biashara ya kimataifa. Wakati huo huo imenasihiwa kuwa mizozo ya kifedha na uchumi isitumiwe kuwa kisingizio cha kutokabilia uharibifu wa mazingira na udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa kama inavyohitajika. Mkutano umehimiza umuhimu wa kuanzishwa ile miradi ya kujenga kile kilichoitwa ‘uchumi wa kijani' wa kudhibiti bora mazingira yalio safi kimataifa.