Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNCTAD azingatia suluhu ya kukabiliana na matatizo ya uchumi na kifedha kwa Afrika

Mkuu wa UNCTAD azingatia suluhu ya kukabiliana na matatizo ya uchumi na kifedha kwa Afrika

Takwimu za UM zimethibitisha kwamba zaidi ya nusu ya idadi ya umma wa Afrika, bado unaishi katika hali ambayo matumizi ya kukidhi mahitaji ya kimaisha, kwa siku, ni chini ya dola moja.

Mzozo wa kiuchumi na fedha uliojiri kwenye soko la kimataifa, ni mgogoro uliopalilia na kudhoofisha zaidi hali ya uchumi wa bara la Afrika, kijumla, uchumi ambao tangu hapo awali ulikuwa unasumbuliwa na ufukara na hali duni, iliochanganyika na wasiwasi wa kisiasa. Supachai Panitchpakdi, KM wa Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), kwenye mazungumzo aliokuwa nayo na Mtayarishaji Vipindi wa Redio ya UM, Jean-Pierre Ramazani, alipendekeza moja ya suluhu ambayo anaamini ikitekelezwa itasaidia kuendeleza hali ya uchumi utakaodumu katika Afrika, ikiwa mataifa ya eneo hili yatashirikiana, kwa ukaribu zaidi.  Alielezea zaidi hoja yake hiyo kwa kulinganisha na fafanuzi za Ripoti Mpya ya UNCTAD juu ya Uchumi wa Afrika:

"Mwunganiko wa shughuli za uchumi miongoni mwa mataifa ya Afrika ni kadhia muhimu sana, kwa sababu kadha: awali, fungamano hizi zikikamilishwa zitaisaidia Afrika kupanua zaidi vyanzo vya uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika kikanda; pili, itasaidia kuanzisha ujuzi wenye kuambatana na mahitaji hakika ya uchumi wa Afrika, hali ambayo itawavutia wawekezaji wa kigeni kuingiza vitega uchumi barani humo, na kuwasilisha mazingira ya mashindano yanayohitajika kusukuma mbele maendeleo. Mwunganiko wa uchumi wa maeneo ya Afrika vile vile utasaidia kuwekeza kwenye ile miradi mikubwa ya kiraia, kwa mfano, miradi ya kusimamia huduma bora za maji, na miradi ya kujenga miundombinu inayofaa kuendeleza, kwa ufanisi, shughuli za kiuchumi zenye natija za muda mrefu."

Sikiliza mazungumzo kamili kwenye idhaa ya mtandao.