Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zimbabwe yashuhudia uzalishaji mkubwa wa kilimo, lakini wasiwasi bado umeselelea juu ya akiba ya chakula

Zimbabwe yashuhudia uzalishaji mkubwa wa kilimo, lakini wasiwasi bado umeselelea juu ya akiba ya chakula

Mashirika mawili ya UM - yaani FAO, linalohusika na chakula na kilimo, pamoja na WFP, linaloshughulikia miradi ya chakula - yamewakilisha bia ripoti ya tathmini halisi juu ya maendeleo ya kilimo katika Zimbabwe.

Ripoti ilibainisha kwamba hali ya wasiwasi imetanda nchini kuhusu akiba maridhawa ya chakula, ijapokuwa uzalishaji wa kilimo na utekelezaji wa mfumo wa sera huru ya uagizishaji wa bidhaa kutoka nje ni huduma zilizofanikiwa kukuwa na kuongezeka katika mwaka huu. Kwa mujibu wa ripoti, kutokana na kiwango kizuri cha mvua ilioanguka katika 2009 nchini humo, mavuno ya mazao makuu ya mahindi yaliongezeka maradufu katika Zimbabwe. Lakini ripoti iliashiria ya kuwa yale mazao ya majira ya baridi, yaani ngano, yanatarajiwa kuwa haba sana katyika majira ya mwaka huu, kwa sababu ya bei ghali ya mbolea, ambayo wakulima walishindwa kuimudu wakati wa kuotesha mazao hayo, na pia kutokana na aina ya mbegu dhaifu zilizotumiwa, ikichanganyika na ukosefu wa ukwasi na huduma isioridhisha ya umeme wa kigeugeu, ambao mara nyingi hutumiwa kumwagilia maji.