Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon alitangaza Ijumatatu alasiri taarifa maalumu ilioleza kuwa aliingiwa wasiwasi na fadhaa, juu ya kufumka kwa fujo na vurugu katika Jamhuri ya KiIslam ya Iran, kufuatia uchaguzi wa uraisi ulioendelezwa nchini humo wiki za karibuni.Alisema alishtushwa na matumizi ya nguvu dhidi ya raia, hali ambayo ilizusha vifo na majeruhi kadha. Aliwasihi wenye madaraka kusitisha, halan, vitendo vyote vya kutumia nguvu dhidi ya raia, na kusimamisha vitisho pamoja na kuwashika watu bila hatia. Alitumai "matakwa ya kidemokrasia ya umma wa Iran yatahishimiwa kikamilifu" na wenye mamlaka.

Ijumanne asubuhi Baraza la Usalama lilianza shughuli zake kwa kupiga kura, kwa kauli moja, ya kuongeza, kwa miezi sita, operesheni za Vikosi vya Uangalizi wa Kusimamisha Mapigano katika Milima ya Jolan (UNDOF). Baada ya hapo, wajumbe wa Baraza walisikiliza fafanuzi za ripoti mpya inayosailia hali katika Guinea-Bissau, iliowasilishwa na Joseph Mutaboba, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Guinea-Bissau, ambaye pia ni mkuu wa Ofisi ya UM ya Kusaidia Ujenzi Amani Guineas-Bissau. Miongoni mwa hatua kadha zilizopendekezwa na ripoti kutekelezwa nchini, kukomesha duru ya fujo na tabia ya kuendeleza makosa ya jinai bila kukhofu adhabu, ni pamoja na ile rai ya kubuni tume maalumu, inayoaminiwa na umma, kufanya uchunguzi kuhusu vyanzo vya vurugu nchini Guinea-Bissau. Alasiri Baraza la Usalama lilizingatia ripoti ya Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati, kuhusu hali katika eneo hilo.

Ripoti ya kati ya mwaka ya Tume ya Wataalamu juu ya Vikwazo dhidi ya Liberia ilitolewa rasmi Ijumanne, kwenye Makao Makuu, na ilizingatia masuala yanayohusu vikwazo vya silaha kwa Liberia, na uwezekano wa kuondoa vizuizi vya usafirishaji wa almasi na mbao nje ya nchi. Vile vile Tume ilifanya mapitio ya vikwazo dhidi ya mali iliozuiliwa kwenye mabenki ya baadhi ya watu anbao pia wamepigwa marufuku kusafiri kwa sababu ya uhusiano wao na Charles Taylor, aliyekuwa raisi wa zamani wa Liberia, ambaye sasa hivi yupo Hague, Uholanzi kukabili mashtaka ya kushiriki kwenye makosa ya vita na jinai dhidi ya utu.

KM leo alishiriki kwenye Taadhima ya Siku ya Tunzo ya UM kwa Wahudumia Jamii, ambapo mchango wa taasisi kadha wa kadha za umma wa kimataifa, kutoka sehemu mbalimbali za dunia, hutambuliwa rasmi kwa mchango wao wa kusaidia kufanya bora maisha ya umma wa kawaida. KM alisema kwenye risala yake kwamba UM ulishatambua kwa muda mrefu ya kuwa utawala bora na usimamizi wenye mpangilio unaofaa umma, ndio vyanzo vinavyotakikana kutekeleza ajenda zinazohusu huduma za maendeleo kwa mafanikio.