Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo la mapigano katika JAK wamehajiri mastakimu: OCHA

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo la mapigano katika JAK wamehajiri mastakimu: OCHA

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti mashambulio yaliotukia Ijumapili alfajiri, tarehe 21 Juni, kwenye mji wa Birao, kaskazini-mashariki ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) yamesababisha idadi kubwa ya wakaazi kuhama kidharura eneo hilo.

Mashambulio yaliendelezwa na moja ya makabila yenye kuunga mkono kundi la UFDR, liliotia sahihi mapatano ya amani kwa  JAK, hali iliosababisha vifo vya raia 3 na kujeruhi askari 6 wa jeshi la taifa. Nyumba 100 pia zilizripotiwa kuunguzwa moto na kuangamizwa vile vile. Watumishi wanaohudumia misaada ya kiutu waliopo Birao walihamishwa kwenye kambi ya vikosi vya Shirika la UM la Ulinzi Amani katika JAK (MINURCAT) kupata usalama. Mjumbe Maalumu wa UM kwa JAK, Victor Angelo, ambaye pia ni mkuu wa Shirika la MINURCAT, Ijumatatu alielekea mji mkuu wa Bangui, katika JAK, kuhudhuria mkutano wa dharura na Raisi, pamoja na maofisa wa serikali, ili kushauriana taratibu za kudhibiti bora kipamoja hali ya usalama nchini, kwenye mazingira yalioripotiwa kuendelea kuharibika.