Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limepokea rasmi katika wiki iliopita maofisa wapya wa polisi 95 kutoka Gambia - wanaume polisi 92 na askari wanawake watatu, askari ambao wanatarajiwa kuenezwa katika sehemu mbalimbali za Darfur baada ya kumaliza mafunzo ya utambulisho yatakayofanyika kwenye mji wa El Fasher.

Asubuhi, B. Lynne Pascoe, Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa alihutubia kikao cha hadhara katika Baraza la Usalama, kusailia hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK), taifa ambalo alilizuru karibuni. Alisema alipokuwepo huko alishuhudia, binafsi, athari za miaka mingi ya hali ya wasiwasi iliotanda nchini, ikichanganyika na vurugu na ukosefu wa usalama. Alisema aliingiwa moyo kuona umma na Serikali bado wana imani kuhusu kazi za UM nchini. Alitoa mwito unaowapendekeza wenye madaraka kuhakikisha uchaguzi utafanyika kwa wakati katika JAK, ili kuepukana na kuzuka kwa pengo la madaraka ya kikatiba, hali ambayo ikijiri ina hatari ya kuanzisha tena fujo nchini. Alisema ripoti ya KM ya karibuni juu ya JAK, ilipendekeza ofisi ya UM ya kujenga amani nchini humo, yaani ofisi ya BINUCA, ianze shughuli zake rasmi 01 Januari 2010. Kadhalika, Baraza la Usalama lilisikia ripoti ya Balozi wa Ubelgiji, Jan Grauls ambaye mwezi uliopita naye pia alizuru JAK, kama mkuu wa Kamati ya Kuchunguza na Kupangilia Mahitaji ya Ujenzi Amani katika JAK. Baada ya hapo wajumbe wa Baraza waliendelea na majadiliano ya faragha kuhusu hali katika JAK.

Alasiri, KM alishuhudia kuapishwa kwa majaji 15 wa Mahakama mpya ya UM ya Kusuluhisha Ugomvi na pia Mahakama ya Rufaa. Majaji hawa waliteuliwa mwanzo wa mwaka na Baraza Kuu, na wapo New York sasa kuhudhuria mafunzo maalumu ya wiki moja na kuhudhuria mikutano kadha katika Makao Makuu. Mahakama hizi zimeanzishwa kukidhi mahitajia ya mfumo mpya wa sheria za ndani katika UM, ambao kwa mara ya awali zitaashughulikia magomvi yanayohusika na kazi katika UM. Taratibu hizi mpya zitaanza kutumika rasmi tarehe 01 Julai (2009).