Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICTR imetangaza kifungo cha miaka 30 kwa mtuhumiwa Kalimanzira

ICTR imetangaza kifungo cha miaka 30 kwa mtuhumiwa Kalimanzira

Mahakama ya UM juu ya Rwanda (ICTR) imetangaza hukumu ya kifungo cha miaka 30, kwa Callixte Kalimanzira, aliyekuwa ofisa Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Rwanda katika 1994, ambaye alipatikana na hatia ya jinai ya mauaji ya kuangamiza makabila, na pia makosa ya kuchochea watu kuendeleza mauaji ya halaiki.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mahakama, Kalimanzira, mnamo tarehe 23 Aprili 1994 aliripotiwa kufuatana na magenge ya wafanya fujo, ikijumlisha wanajeshi na polisi, ambao walielekea kwenye kilima cha Kibuye, katika wilaya ya Butare, walipokuwepo maelfu ya raia wahamiaji wenye jadi ya KiTutsi, waliokusanyika huko kupata hifadhi, umma ambao ulishambuiliwa na magenge hayo na kuuawa. Tukio hili lilitafsiriwa na Mahakama kuwa ni msiba mkubwa kabisa wa kiutu kutukia katika eneo la Maziwa Makuu. Mahakama ilisema mashambulio yalifanikiwa kutendeka kwa sababu ya mchango wa Kalimanzira, ambao Mahakama imethibitisha, pasipo shaka yoyote, ulimhusisha mtuhumiwa kikamilifu kwenye makosa ya jinai ya mauaji ya halaiki yaliofanyika Kabuye.