Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti karibuni limeshuhudia idadi kubwa ya waliokuwa waasi wa Ki-Hutu wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR) kurejea makwao Rwanda. Wafuasi wa zamani 57 wa kundi la FDLR na wahamiaji wengine 26 waliokuwa wakiishi kwenye eneo la wasiwasi na mapigano la kaskazini-mashariki, katika JKK, walirejea Rwanda, kwa hiyari, wakisaidiwa na UM. Kadhalika, tangu mwanzo wa 2009, watoto wapiganaji wa umri mdogo 1,650 ziada nao pia walihamishwa kutoka majeshi ya mgambo na kurudishwa kwa wazee wao. MONUC ilieleza ya kuwa vikosi vya kulinda amani vya UM vilianzisha utaratibu unaotumia werevu maalumu, unaowawezseha kutoa hadhari ya mapema, na kufuatilia kwa ukaribu zaidi, vitimbi haramu vya makundi yenye silaha yaliopo Kivu Kaskazini, pale wanapoendesha operesheni zao za kijeshi shirika na vikosi vya taifa vya JKK. Operesheni hizi ziliimarishwa zaidi wiki hii baada ya kufunguliwa kituo kingine cha 8 kinachotumiwa kuratibu shughuli zao hizo.

Duru ya pili ya mazungumzo ya upatanishi baina ya Serikali ya Sudan na kundi la waasi la JEM (Justice and Equality Movement) yaliofanyika kwenye mji wa Doha, Qatar kuanzia tarehe 27 Mei (2009), sasa yamesimamishwa, kwa muda, na yanatazamiwa kuanza tena mwisho wa mwezi Julai. Makundi husika yalivunja mazungumzo ili kuyawezesha kuzingatia zaidi masuala mawili muhimu, yaliojumuishwa kwenye meza ya mashauriano, yaani suala la kusimamisha mapigano, mkabala na ile rai ya kubadilishana wafungwa waliotekwa kwenye mapigano. Katika duru ya sasa ya mashauriano, JEM inapendekeza wafuasi wao wafungwa waachiwe huru kabla ya maafikiano ya amani kukamilishwa ili kusitisha uhasama, wakati Serikali inasisitiza uhasama ukomeshwe kikamilifu kwanza, kabla ya mateka kuwachiwa huru. Mnamo kipindi cha kusimamishwa mashauriano, kwa muda, juhudi za upatanishi zitaendelea, na wadau wote wanaohusika na mpango wa amani wataendelea kushauriwa, panapohitajika.

Tangu Ijumatano ya wiki hii, Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro alianza ziara rasmi Norway, ambapo alijihusisha na masuala yanayofungamana na utekelezaji wa sheria juu ya haki ya kimataifa, hususan namna inavyotumiwa kuwakinga watoto wa kike na wanawake na vitendo vya kutumia nguvu na mabavu dhidi yao, na namna zinavyotekelezwa kuwakinga watoto dhidi ya utenguzi wa haki hizo kimsingi. Alkhamisi, NKM alitoa hotuba muhimu, mbele ya wawakilishi waliohudhuria kikao cha 29 cha Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Baraza la Mataifa ya Ulaya, ambayo iliwasilisha ujumbe maalumu kuhusu suala la matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake. Alisema uchunguzi ulioendelezwa kimataifa juu ya mada hii umethibitisha ya kwamba nusu ya wanawake wanaofariki kutokana na mauaji, huuliwa ama na waume zao wa sasa au wale wa zamani, na hata mara nyengine huuawa na wanaume marafiki. Alisema kukomesha jinai hii ya kutumia mabavu dhidi ya wanawake kutahitajia kubuniwa sheria mpya kwenye mataifa husika, au kuimarisha kanuni zilizokuwepo sasa hivi kuwanusuru wanawake na watoto wa kike na udhalilishaji wa kijinsiya. Wakati huo huo, aliendelea kusema, angelipendelea kuona mawazo na itikadi za kikale zinarekibishwa, zile itikadi zinazowahamasisha watu kuridhia, kusamehe au kutojali vitendo vya ukatili vya kutumia nguvu dhidi ya wanawake. Alitilia mkazo kwamba UM upo tayari kusaidia kama inavyostahiki, kuleta marekibisho kwenye huduma za kuwakinga wanawake na watoto wa kike na udhalilishaji wa kijinsiya. Kadhalika, wakati NKM alipokuwa Norway alifanya mikutano ya pande mbili kadha, ikijumlisha mazungumzo maalumu na waziri wa sheria wa taifa hilo la Skandinavia, pamoja na kukutana na Naibu-Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya. NKM Migiro alitazamiwa kurejea New York mwisho wa wiki.