Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanariadha wa kimataifa kushiriki kwenye miradi ya kupiga vita njaa ulimwenguni

Wanariadha wa kimataifa kushiriki kwenye miradi ya kupiga vita njaa ulimwenguni

Jarno Trulli na Timo Glock, madereva wa mashindano ya mbio za gari, wenye kuwakilisha kampuni za Panasonic na Toyota, wanatazamiwa kuvalisha na kupamba gari zao na alama ya kitambulisho ya lile Shirika UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP), pale watakaposhiriki kwenye mashindano ya gari Uingereza mnamo Ijumapili ijayo.

Madhumuni yao ni kusaidia kueneza kampeni ya UM ya kuzindua hisia ya kimataifa juu ya umuhimu wa kuchangisha fedha zinazotumiwa kuwasaidia watoto wa skuli za msingi milioni 20 katika nchi 68, kupata chakula kila siku. Kwa mujibu wa ripoti za UM watoto wa skuli za msingi milioni 66 duniani huwa wanahudhuria masomo, kila siku, wangali pia wanateswa na tatizo sugu la njaa. Kampeni hii ya WFP, inayojulikana kwa umaarufu kama kampeni ya "Jaza Chakula Bakuli" hufadhiliwa fedha na Abdul Lateef Jameel wa Saudi Arabia, mfanyabiashara huru mkubwa ulimwenguni anayeuza magari ya Toyota.