ICC yathibitisha kesi kwa aliyekuwa naibu-raisi wa JKK

17 Juni 2009

Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) imethibitisha kuwa kuna ushahidi wa kuridhisha wa kuanzisha kesi ya kumtuhumu Jean-Pierre Bemba Gombo, aliyekuwa naibu-raisi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), kwamba alishiriki kwenye makosa ya vita na jinai iliotengua haki za kiutu.

Bemba anatazamiwa kushtakiwa rasmi katika tarehe itakayotangazwa baadaye. Majaji wa ICC wanaamini Bemba alikuwa na "dhamira isioepukika ya kuendeleza vitendo vya uhalifu" katika 2002, pale alipowaamrisha wafuasi wa jeshi la mgambo aliokuwa akiliongoza la Movement for the Liberation of Congo (MLC), kuingia ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kumhami Ange-Félix Patassé, kiongozi wa taifa aliyekuwa mashakani. Kwa mujibu wa ICC wapiganaji wa MLC wakati huo walituhumiwa kuhusikana na makosa ya vita na jinai mbalimbali dhidi ya utu, wakiongozwa na Bemba. Makosa ya uhalifu wanaotuhumiwa nayo wapiganaji wa MLC hujumlisha vitendo vya kunajisi kimabavu, mauaji na unyanganyi wa mali kwa nguvu. ICC ilisema ilivyokuwa haina ushahidi unaoaminika kuhusu makosa mengine iliopokea imelazimika kutoruhusu mashitaka hayo mahakamani, yakijumuisha makosa ya kutesa. Bemba alishikwa mwezi Mei 2008 na kuhamishwa kwenye Mahakama ya ICC mwezi Julai.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud