Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Kwenye mkutano na waandishi habari uliofanyika kwenye Makao Makuu, KM Ban Ki-moon alitangaza kumteua rasmi Raisi mstaafu wa Marekani, Bill Clinton kuwa Mjumbe Maalumu wa UM kwa Haiti. Mkutano ulihudhuriwa na Raisi Clinton pamoja na Waziri wa Nchi za Kigeni wa Haiti, Alrich Nicolas. Clinton aliwaambia wanahabri ya kwamba licha ya dhoruba kadha wa kadha zilizopiga Haiti mwaka uliopita na kusababisha uharibifu mkubwa ndani ya nchi, sasa hivi taifa hilo limo kwenye mazingira yenye matumaini ya kufufua, kwa mafanikio, huduma za kiuchumi na kijamii nchini.

Ripoti ya KM juu ya Darfur, inayowakilishwa kwenye Baraza la Usalama kila mwezi, imeeleza mapigano yamekithiri mpakani baina ya Chad na Sudan, hali iliosababisha ukosefu mkubwa wa usalama. Ripoti ilibainisha pia kwamba jumla ya wanajeshi wanaotakiwa kuongoza operesheni za UNAMID katika eneo la uhasama sasa hivi imefikia askari 13,000, kati ya jumla ya wanajeshi 19,600. Lakini vikosi hivi bado havijapokea zana na vifaa kamili vinayohitajika kuendesha shughuli zao kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Usalama, hususan zile helikopta 18 zilizoahidiwa na jumuiya ya kimataifa kutumiwa UNAMID. Kadhalika ripoti ilisema uhuru wa majeshi ya UNAMID kwenda watakapo umedhibitiwa na Serikali ya Sudan; na vitendo vya utekaji nyara magari ya wahudumia misaada ya kihali ikichanganyika na uharamia unaoendelea, ni mambo yanayohatarisha maisha ya watumishi wa UM. Kwa mujibu wa ripoti, zile juhudi za mashirika ya kimataifa kugawa misaada ya kiutu katika Darfur, sasa zinaonyesha ishara ya kutengenea, baada ya Serikali kuwafukuza nchini baadhi ya watumishi na mashirika yasio ya kiserikali ya kimataifa.

Wakati huo huo, Ameera Haq, Mratibu wa UM juu ya Misaada ya Kiutu kwa Sudan ameshtumu mashambulio maututi yalioendelezwa na wapiganaji wa kikabila Ijumaa iliopita, katika Mto Sobat, dhidi ya matishali makubwa yaliokuwa yamechukua shehena ya chakula kugaiwa umma muhitaji na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP). Mashambulio haya yalitukia karibu na kijiji cha Nyariem, kiliopo katika Jimbo la Nile ya Juu, tukio ambalo lilizusha mapigano ya muda, kati ya washambulizi na polisi walinzi wa Serikali ya Sudan Kusini waliokuwa wakishindikiza matishali hayo. Idadi ya polisi na wapiganaji wa kikabila waliouawa kwenye tukio hili haijatambulikana bado.

Naibu KM juu ya Opereshani za Amani za UM, Alain Le Roy anazuru Liberia kwa sasa, ambapo alikutana na maofisa wa ngazi za juu wa Shirika la Kulinda Amani Liberia (UNMIL). Ijumanne alitazamiwa kufanya mazungumzo rasmi na Raisi wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.

Ripoti ya KM juu ya Liberia, iliotolewa Ijumatatu, imebainisha hali huko bado ni ya kuregarega licha ya kuwa taifa, kwa ujumla, limepiga hatua katika kurudisha utulivu na amani kufuatia mapigano ya miaka 14. Washirika wote wa kimataifa waliombwa kuendelea kuisaidia Liberia kihali, ili kuiwezesha kuimarisha vizuri zaidi amani na kudumisha utulivu wa muda mrefu nchini. Kadhalika ripoti ya KM ilipendekeza jumla ya vikosi vya Shirika la UM Kulinda Amani Liberia (UNMIL) ipunguzwe mnamo mwezi Mei 2010 - kutoka askari 10,231 hadi 8,202. Idadi ya walinzi amani 8,202 ndio itayobakia mpaka wakati wa uchaguzi, unaotazamiwa kufanyika nchini katika 2011. Uondoshaji wa mwisho wa vikosi vya UNMIL kutoka Liberia utategemea matokeo ya tathmini itakayofanyika baadaye na Serikali, UM na wadau wengineo, ikijumlisha pia Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kufuatia mashauriano yao juu ya suala hilo.

Asubuhi Baraza la Usalama limekutana kusikiliza ripoti ya fafanuzi za Balozi Yukio Takasu wa Ujapani kuhusu kazi za Kamati ya 1737 juu ya Vikwazo dhidi ya Iran. Baadaye Baraza lilijadilia suala la kuongeza muda wa Shirika la Uangalizi la UM juu ya Kusitishwa Mapigano katika Georgia (UNOMIG). Alasiri Baraza la Usalama lilikutana tena kuzungumzia suala hilo na wajumbe wa Baraza walishindwa kupitisha azimio la kuongeza muda wa shughuli za UNOMIG kwa sababu ya kura ya kupinga iliotiwa na mwakilishi wa Shirikisho la Urusi. Mataifa ya Uchina, Libya, Uganda na Vietnam hayakupiga kura. Shughuli za UNOMIG zilianzishwa miaka 16 iliopita na Baraza la Usalama, kwa makusudio ya kusimamia kuacha mapigano baina ya vikosi vya Serikali na wapiganaji wa jimbo linalotaka kujitenga la Abkhazia.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay ametoa mwito maaulumu uitakayo Israel kuregeza vikwazo dhidi ya shughuli za kuingiza na kutoa bidhaa katika eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza. Hali hiyo, alisema Pillay, inakiuka haki za binadamu. Alitilia mkazo umuhimu wa Serikali ya Israel pia kushirikiana, kikamilifu, na wajumbe wa tume ya uchunguzi ya Baraza la Haki ya Binadamu iliodhamaniwa kufafanua taathira za mashambulio ya Israel katika Ghaza. Tume inaongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini.