Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WHO ahimiza haki kwenye sera za kimataifa

Mkuu wa WHO ahimiza haki kwenye sera za kimataifa

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dktr Margaret Chan aliwaambia wajumbe wa kimataifa, waliohudhuria warsha maalumu uliofanyika Makao Makuu ya UM, kuwacha ile tabia ya “kuamini, bila kuelewa, madai yanayojigamba ustawi wa uchumi na natija zake kimataifa ndio mambo yatakayofanikiwa kumaliza na kuponya matatizo yote ya maisha duniani.”

Aliyasema hayo kwenye hotuba ya ufunguzi wa majadiliano yanayozingatia "taratibu za kuendeleza mbele afya ya jamii kwenye ulimwengu uliovamiwa na migogoro". Kwenye risala yake, Dktr Chang alisisitiza wakati umewadia, kwa jumuiya nzima ya kimataifa, kubuni mfumo mpya ulio wa haki, utakaohakikisha hadhi ya afya itatumiwa kuwa kigezo cha msingi wa kutathminia huduma za maendeleo yalivyo kitaifa na baina ya mataifa, kwenye mazingira ya ulimwengu unaojigamba umestaarabika, hasa katika karne hii ya ishirini na moja.

Mkutano ulifunguliwa rasmi na KM Ban Ki-moon, ambaye alihadharisha kwenye hotuba yake ya kuwa tangazo la WHO liliothibitisha kuripuka kwa janga la maambukizi ya homa ya mafua ya H1N1 kimataifa ni tukio lilionyesha wazi kabisa ulazima wa kukuza ushirikiano wa pamoja katika kukabiliana na matatizo ya afya. Alipendekeza uwekezaji ukuzwe kwenye sekta ya afya, hatua ambayo inaaminiwa itasaidia kupunguza gharama zitakazozuka dhidi ya watu na uchumi, pindi patakosekana kadhia hiyo kwa sababu ya kuzubaa kwa kimataifa.