Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM amemteua Moustapha Soumaré wa Mali kuwa Naibu Mjumbe Maalumu mpya atakayeshughulikia kitengo kinachohusika na Ufufuaji wa Huduma za Jamii na Uchumi na Utawala Bora kwenye Shirika la UM juu ya Operesheni za Amani Liberia (UNMIL). Soumaré pia atashika wadhifa wa Mratibu Mkaazi wa UM na Mshauri wa Misaada ya Kiutu wa UM kwa Liberia.

Shirika la UM juu ya Operesheni za Kulinda Amani katika JKK (MONUC) limeripoti vikosi vya Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati vinatazamiwa kujiunga na wanajeshi wa JKK na Uganda, kwenye operesheni za pamoja za kuwatoa mafichoni waasi makatili wa Uganda wa kundi la LRA waliojizatiti kwenye maeneo ya JKK. Taarifa hii ilitangazawa baada ya kumalizika mkutano uliofanyika Kisangani, jana Alkhamisi, ambapo maofisa wa kijeshi, pamoja na wataalamu wanaohusika na vikosi vya upelelezi walihudhuria na kufanya mapitio juu ya utaratibu wa vikosi vya JKK kuwakomoa kutoka mafichoni katika jimbo la kaskazini-mashariki la Province Orientale waasi wa LRA, operesheni ambazo zinaungwa mkono na vikosi vya kulinda amani vya UM viliopo nchini. Kamanda Mkuu wa vikosi vya MONUC, Jenerali Babacar Gaye naye pia alihudhuria kikao hiki muhimu.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza taarifa yenye kukanya yale madai yaliochapishwa na vyombo vya habari, katika tarehe 11 na 12 Juni 2009, yanayojigamba mashirika manne ya kigeni yasio ya kiserikali, yaliofukuzwa Sudan miezi iliopita ati yamepatiwa idhini na wenye madaraka kurejea nchini kuendeleza shughuli za kuhudumia misaada ya kiutu kwa raia muhitaji. Kwa mujibu wa Ofisi ya Msemaji wa KM (OSSG) mashirika hayo, yalionakiliwa kwenye vyombo vya habari kadhaa, ni jumuiya mpya zilizosajiliwa rasmi kuwa ni mashirika yasio ya kiserikali ya kimataifa (INGO) yalioruhusiwa na Sudan kufungua operesheni mpya za kugawa misaada ya kihali nchini kwa raia wanaohitajia misaada muhimu ya kunusuru maisha.

Mkuu mpya wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP), Helen Clark aliripotiwa Ijumaa kuzuru Jamhuri ya Kideomkrasi ya Kongo (JKK), na kukutana na viongozi wa serikali pamoja na wawakilishi wa tawala za kienyeji. Vile vile alizuru miradi ya UNDP inayoendelezwa mjini Kinshasa na katika eneo la mashariki. Kabla ya hapo, mnamo Alkhamisi, Bi Clark alizuru Liberia na alikutana na Raisi Ellen Johnson-Sirleaf ambaye alimuahidi UNDP itaendelea kuisaidia Liberia kuimarisha huduma zake za ujenzi wa amani kufuatia kipindi kirefu cha vurugu nchini humo. Mkuu wa UNDP anatazamiwa kuelekea Ethiopia kutathminia miradi ya maendeleo huko, halkadhalika.