Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya mafua ya A(H1N1) yatambuliwa na WHO kuwa janga la ugonjwa wa kuenea kimataifa

Homa ya mafua ya A(H1N1) yatambuliwa na WHO kuwa janga la ugonjwa wa kuenea kimataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ilani maalumu yenye kuthibitisha kwamba Homa ya Mafua ya A(H1N1) sasa inatambuliwa rasmi kuwa ni janga la ugonjwa wa kuenea kimataifa - hii ni aina ya ilani ambayo inatangazwa tena kwa mara ya kwanza na WHO baada ya kipindi cha miaka 40.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO, Dktr Margaret Chan aliwasilisha tangazo hilo Alkhamisi magharibi mjini Geneva, baada ya kamati ya dharura kumaliza kikao maalumu juu ya homa ya mafua ya H1N1, kama ifuatavyo:

"Kwa kigezo cha ushahidi uliokusanywa sasa hivi, na uchanganuzi wa wataalamu wa kimataifa, kuhusu virusi vya homa ya mafua, kwa ujumla, tunaweza kuthibitisha kihakika kwamba ulimwengu sasa umetomea kwenye mkondo wa mazingira yaliovamiwa na janga la kuenea kimataifa kwa ugonjwa wa A(H1N1). Kwa hivyo, kuambatana na ushahidi huo wa kisayansi, nimeamua rasmi kupandisha juu kipimo cha tahadhari ya maambukizi ya homa ya H1N1, kutoka daraja ya 5 hadi daraja ya 6. Hivi sasa ulimwengu umeingia kwenye mkondo wa 2009 uliovamiwa na janga la ugonjwa wa homa ya mafua ya H1N1."