Skip to main content

WFP kuonya, mizozo ya fedha duniani hupalilia njaa kwa mafukara

WFP kuonya, mizozo ya fedha duniani hupalilia njaa kwa mafukara

Ripoti mpya ya uchunguzi, iliotolewa na Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) leo imeeleza ya kuwa mzozo wa kifedha uliozuka katika miezi ya karibuni, katika soko la kimataifa, umeathiri zaidi watu maskini na wale wenye njaa - umma ambao hali yao ya kimaisha inaashiriwa itaharibika zaidi katika siku zijazo.

Ripoti ilitolewa wakati mmoja na kuanza mjini Roma kwa mkutano wa mawaziri wa huduma za maendeleo kutoka nchi wanachama wa jumuiya ijulikanayo rasmi kama Kundi la G-8, wajumbe ambao huwakilisha zile nchi zenye maendeleo makubwa ya viwandani. Uchunguzi wa WFP juu ya athari za mzozo wa fedha uliendelezwa katika mataifa ya Armenia, Bangladesh, Ghana, Nicaragua na Zambia, ambapo ilikadiriwa umma wenye kuishi na matumizi ya chini ya dola 2 kila siku, ndio unaoteseka na kuumia zaidi kihali. Mkurugenzi Mkuu wa WFP, Josette Sheeran, ameziomba Serikali wanachama "kukuza miradi inayotakikana kukidhi bora mahitaji ya kimsingi ya umma huo, hasa katika kipindi muhimu tuliokuwemo sasa hivi. Uchunguzi wa WFP uligundua makundi ya umma yalioathirika zaidi na mzozo wa kifedha hujumuisha wafanyakazi wasio na ujuzi, wanaoishi kwenye miji, na zile jamii zinazotegemea malipo kutoka nchi za kigeni, pamoja na wafanyakazi walioachishwa vibarua katika sekta za usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, na pia wale raia wanaotumikia sekta za utalii na kwenye migodi.