Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inahadharisha, Pembe ya Afrika inakabiliwa tena na mwaka wa njaa

WFP inahadharisha, Pembe ya Afrika inakabiliwa tena na mwaka wa njaa

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetoa onyo maalumu leo hii kutoka ofisi zake ziliopo Roma, Italiana, linalohadharisha kwamba mamilioni ya watu wanaoishi katika Pembe ya Afrika wanakabiliwa, kwa mara nyengine tena, na mchanganyiko maututi wa ukame ulioselelea, mvua haba na mizozo isiokwisha, katika mazingira ambayo bei ya chakula, hususan kwenye nchi nyingi zinazoendelea, nayo pia bado inaendelea kuwa ya juu kabisa.

Zaidi ya hayo, athari za migogoro ya fedha kwenye soko la kimataifa, inatishia kuongeza matatizo ya njaa na kusababisha watu kukosa matumaini kwa siku zijazo, ilisema WFP. Hivi sasa WFP inahudumia chakula watu milioni 17 katika mataifa ya Usomali, Kenya, Ethiopia, Uganda kaskazini na Djibouti, lakini inakhofia idadi ya umma huo muhitaji itaongezeka katika wakati misaada inayohitajika kuendesha operesheni zake inaendelea kudidimia, na inahitajia sasa hivi kufadhiliwa, kidharura, na wahisani wa kimataifa msaada wa dola milioni 450 ili kuendesha shughuli zake katika miezi sita ijayo.