Skip to main content

Mapigano ya Mogadishu yasababisha raia 117,000 kung'olewa makazi: UNHCR

Mapigano ya Mogadishu yasababisha raia 117,000 kung'olewa makazi: UNHCR

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti mnamo mwisho wa wiki iliopita maelfu ya raia walilazimishwa kuyahama mastakimu yao, kufuatia mapigano makali yalioshtadi kwenye mitaa ya mji mkuu wa Mogadishu, Usomali, hali ambayo ilisababisha umwagaji damu mkubwa kabisa. UNHCR inakadiria watu 117,000 waling\'olewa makazi kwa sababu ya mapigano haya.

Kadhalika, imeripotiwa watu 200 waliuawa katika mwezi Mei kwa sababu ya mapigano. William Spindler, msemaji wa UNHCR aliwaambia waandishi habari Geneva kwamba "hali ya vurugu liliozuka majuzi Mogadishu, linakoroga zaidi hali duni ya maisha iliowakabili wakazi wa mji huo":

"Jinsi namna raia wanavyoathiriwa na kusumbuliwa na mapigano ya Mogadishu, ni hali isiokubalika hata kidogo na jumuiya ya kimataifa .. kwa sababu makundi yanayopigana katika Mogadishu yameshindwa hata kuzingatia usalama wa raia, vitendo ambavyo kisheria vinatengua dhahiri, shahiri, kanuni zote za kiutu za          kimataifa na kuharimisha haki za binadamu." Alisema UNHCR imeyasihi makundi yanayohasimiana katika mji wa Mogadishu kuhakikisha usalama na kuhishimu hifadhi ya raia, kama ilivyoidhinishwa na sheria za kimataifa, hasa ilivyokuwa asilimia kubwa ya watu waliong'olewa makazi hujumlisha wanawake na watoto wadogo, umma ambao ulionekana ukihajiri mastakimu yao wakati wamebeba vikorokoro vichache vya kumudu maisha, na kulazimika pia kuvumilia mazingira magumu kabisa.