Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Taarifa ya Baraza la Usalama kwa vyombo vya habari, iliotolewa Ijumanne ya leo, ilipongeza maendeleo yaliojiri karibuni nchini Burundi katika kutekeleza mpango wa amani, hasa ule mpango wa kunyanganya silaha kundi la waasi la FNL, kundi ambalo pia sasa hivi limejiandikisha rasmi kutambuliwa kuwa ni chama cha kisiasa, na limeridhia kujiunganisha na taasisi za kitaifa, na kuwaachia wale watoto wapiganaji waliohusiana nao hapo kabla.

Vile vile, leo asubuhi, Baraza la Usalama lilifanyisha vikao viwili maalumu - vya hadhara na faragha - kuzingatia hali, kwa ujumla, katika Burundi. Mjumbe Mtendaji wa KM kwa Burundi, Youssef Mahmoud alielezea mafanikio yaliopatikana nchini kwenye utekelezaji wa Mapatano ya Jumla ya Kusitisha Mapigano, na katika matayarisho ya uchaguzi ujao wa 2010. Lakini Mjumbe wa KM alihadharisha ya kuwa juu ya kupatikana mafanikio hayo ya kisiasa kuna wasiwasi bado kuhusu vitimbi vya polisi, watumishi wa idara za ulinzi na usalama, wakichanganyika na maofisa wa serikali za kienyeji ambao wanaendelea, mara kwa mara, kusambaratisha na kuvuruga shughuli za vyama vya siasa vya upinzani. Alisema matatizo mawili magumu juu ya usalama wa taifa yanayokabili juhudi za kuimarisha amani katika Burundi kwa sasa yanafungamana na shughuli za kukamilisha upokonyaji silaha, kutoka wale wapiganaji wa zamani ambao wanahitajia kujumuishwa kwenye shughuli, za kudumu, za kiuchumi na jamii taifani mwao. Wakati huo huo KM amependekeza madaraka ya Ofisi ya UM Kuunganisha Huduma za Amani Burundi yasibadilishwe, na alitaka hadhi yake ya kisheria iendelee kutambuliwa kama ilivyo sasa hadi mwisho wa 2009.

Henry Anyidoho, Naibu Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) asubuhi alizuru kijiji kimoja katika Darfur Kusini ambapo alikutana, kwa mazungumzo, na viongozi wa kijadi waliowakilisha wanakijiji 1,500. Tuliarifiwa fungu kubwa la wahamiaji hawa lilirejea makwao karibuni kutoka kambi za wahamiaji wa ndani, walipokuwa wakiishi kwa muda mrefu, maeneo yaliopatiwa hifadhi na vikosi vya kimataifa. Mazungumzo yao yalizingatia zaidi suala la kuwahamisha tena wanakijiji, na kuwapeleka kwenye maeneo mengineyo ambapo hali ya usalama ni madhubuti. Kadhalika, leo hii, Naibu Kamanda Mkuu wa Vikosi vya UNAMID, Meja Jenerali Duma Dumisani Mdutyana, alizuru kambi ya Zam Zam iliopo Darfur Kaskazini, kambi ambayo inahudumia makazi ya muda wahamiaji wa ndani. Jenrali Mdutyana alipatiwa maelezo kuhusu viguzo vinavyosambaratisha shughuli za amani kwenye eneo husika la Darfur.