Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Helen Clark, Mkuu wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) Ijumanne ataanza ziara ya awali katika Afrika tangu kuchukua madaraka ya kuiongoza taasisi hiyo ya UM. Atayatembelea mataifa ya Liberia, JKK na Ethiopia kutathminia maendeleo kwenye utekelezaji wa miradi ya UNDP huko, na pia atakutana na maofisa wa vyeo vya juu wa serikali za mataifa anayoyazuru.

Baraza la Usalama asubuhi lilifanyisha mkutano wa hadhara, kuzingatia hali katika Sierra Leone. Mjumbe Mtendaji wa KM kwa Sierra Leone, Michael von der Schulenburg kwenye ripoti yake mbele ya wajumbe wa Baraza alielezea mafanikio yaliopatikana nchini katika juhudi za kuimarisha amani, baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kusita katika Sierra Leone mnamo 2002. Alisema Serikali na makundi ya upinzani yanapaswa kupongezwa juu ya namna walivyokabiliana na fujo zilizozuka nchini karibuni - tukio la hatari ambalo liliweza kuzimwa bila ya machafuko kuenea zaidi nchini. Alieleza kwamba makundi yote yaliotia sahihi mapendekezo ya Taarifa ya Pamoja yameonyesha ujasiri wa kutambua majukumu walionayo kujenga, kwa pamoja, Sierra Leone iliostawi na yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia. Alikumbusha mashirika ya UM katika Sierra Leone yameandaa utaratibu unaojulikana kama Mtazamo wa Pamoja, wa kutumiwa kuisaidia serikali kuwasilisha mageuzi nchini yanayogharamia dola milioni 350 katika kipindi cha miaka minne ijayo, baina ya 2009 mpaka 2012. Aliyaomba Mataifa Wanachama ya UM NA Baraza la Usalama kuchangisha msaada wa fedha hizo pamoja na mchango wa kisiasa ili kusaidia kutekeleza mradi wa maendeleo katika Sierra Leone.

KM Mdogo wa UM juu ya Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe leo ameanza ziara ya kutembelea nchi sita za Afrika Magharibi na Kati - ikijumlisha Senegal, Ghana, Nigeria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sierra Leone na Guinea-Bissau. Anatazamiwa kukutana kwa mashauriano na viongozi wakuu wa mataifa hayo, pamoja na wale walio nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS). Miongoni mwa masuala yatakayopewa umuhimu kwenye mazungumzo yao ni pamoja na maendeleo ya kisiasa hivi sasa kieneo, na mchango wa UM katika kuimarisha utulivu na amani kwenye ukanda husika.

Mwisho wa wiki iliopita Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK pamoja na Waziri wa Ulinzi wa JKK walizuru majimbo ya Kivu, katika mashariki ya nchi, kutathminia maendeleo kuhusu zile operesheni za pamoja za vikosi vya UM vya MONUC na jeshi la taifa, za kuwang'oa kutoka mafichoni makundi haramu ya waasi wenye silaha. Doss na Waziri wa Ulinzi walikutana na makamanda wa UM na kutoka jeshi la taifa la JKK, na walisailia ushirikiano na uratibu wa operesheni zao za kuhakikisha raia wanaosumbuliwa na kuteswa mara kwa mara kwenye vijiji vyao na waasi haramu huwa wanapatiwa hifadhi madhubuti na inayoaminika.

Wakati huo huo MONUC imetangaza taarifa ya kuunga mkono uamuzi uliopitishwa Ijumaa, kwenye mji wa Kisangani, na mahakama ya kijeshi kwa kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa wapiganaji waasi watano, waliokutikana na makosa ya kujamii kihorera waathirika wanawake 135, ikichanganyika pia na makosa mengine ya kijinsiya. Hukumu vile vile iliowataka watuhumiwa hao kutoa fidia ya fedha kwa waathiriwa wanawake wa makosa ya kunajisiwa kimabavu.

Mkutano wa kimataifa kuzingatia ajenda ya majadiliano ya mkutano ujao kuhusu udhibiti bora wa mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, unaofanyika Bonn, Ujerumani chini ya uongozi wa UM, asubuhi ya leo umeingia wiki ya pili ya majadiliano. Wawawkilishi wa nchi wanachama waliwakilisha maoni yao ya hapa na pale juu ya ratiba iliopendekezwa kuzingatiwa katika mkutano mkuu wa Copenhagen utakaofanyika mwezi Disemba. Na kuanzia kesho wajumbe wa kimataifa watawakilisha mapendekezo ya kina, kwa dhamira ya kuyajumuisha kwenye maafikiano ya jumla juu ya udhibiti bora wa taathira za mabadiliko ya hali ya hewa, yanayotarajiwa kukamilishwa kwenye kikao cha Copenhagen.