Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shambulio la bomu liliotukia Ijumaa kwenye msikiti wa wilaya ya Dir ya Juu katika Pakistan, liliosababisha vifo vya watu 30, ni kitendo karaha kilicholaumiwa vikali na KM. Kwenye taarifa juu ya tukio hili KM alisisitiza, kwa mara nyengine tena kwamba vitendo vyote vya kutumia mabavu na fujo za kihorera dhidi ya raia ni uhalifu unaostahiki kupingwa na kulaaniwa kimataifa. Aliwatumia mkono wa pole kwa aila zote za waathirika wa tukio hilo pamoja na Serikali ya Pakistan.

Vile vile KM alitoa taarifa yenye kueleza kuchukizwa sana na ripoti kuhusu mauaji ya Baciro Dabo, mgombea uchaguzi ujao wa uraisi katika Guinea-Bissau pamoja na mauaji ya Mbunge Helder Proenca, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, na kuchukizwa pia na mauaji ya watu wengine kadhaa nchini. Alisema mwelekeo huu hatari wa mauaji ya watu mashuhuri katika Guinea-Bissau unamtia wasiwasi juu ya utulivu wa taifa. Alikumbusha vitendo hivi vya kihalifu vilizuka muda mdogo tu baada ya kuuliwa Raisi João Bernardo Vieira pamoja na Jenerali Tagme Na Waie, hali ambayo alisisitiza imerejesha nyuma zile juhudi muhimu za kufufua utaratibu wa kutii sheria za nchi na mfumo wa kidemokrasia. Aliwahimiza wananchi wa Guinea-Bissau kutoruhusu mauaji haya kuzorotisha matayarisho ya uchaguzi ujao wa uraisi.

Baraza la Usalama lilifanyisha kikao cha hadhara leo asubuhi ambapo Luis Moreno-Ocampo, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) aliwakilisha ripoti ya kuendelea kwa uchunguzi wa ofisi yake kuhusu makosa ya uhalifu wa vita yaliodaiwa kufanyika katika Darfur. Alisema mnamo miezi sita ijayo, ofisi ya Mwendesha Mashtaka itaendelea kufuatilia vitendo vya wale wenye dhamira ya kuendeleza makosa ya jinai, pamoja na kufuatailia juhudi za kuwashika watoro wanaosakwa na Mahakama. Alisema kwa sasa hana azma ya kufungua kesi mpaya katika kipindi hicho, na kutilia mkazo ya kuwa, kwa ufahamivu wake, Serikali ya Sudan ina jukumu na dhamana la kisheria kuhakikisha inawashika raia walioshtakiwa na ICC.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kuwepo dalili za kutia moyo Zimbabwe baada ya kubainika idadi ya vifo vya watu walioambukizwa na kipindupindu nchini kuteremka. Wagonjwa wa kipindupindu 4,000 ziada walisajiliwa kufariki Zimbabwe katika miezi iliopita. Wakati huo huo OCHA imetahadharisha kwamba kutahitajika juhudi za pamoja kuyadhibiti vyema maradhi katika baadhi ya sehemu za Zimbabwe, kwa sababu kumepokelewa ripoti zinazobainisha bado kuwepo kwa idadi kubwa ya watu walioambukizwa na kipindupindu. OCHA inasema matatizo ya upungufu wa maji safi na salama, na vile vile ukosefu wa mastakimu safi katika sehemu nyingi za nchi ni masuala ambayo yameshindwa kukabiliwa kidharura kama inavyotakikana na wataalamu wa kimataifa, hali ambayo ndio iliozusha mripuko wa kipindupindu kwenye miezi ya nyuma.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza taarifa maalumu inayopendekeza matumizi ya ile chanjo ya kuzuia ugonjwa hatari wa kuharisha, kote duniani, maradhi yanayosumbua zaidi watoto wachanga. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo kila mwaka huua watoto wachanga 500,000, na asilimia 85 ya vifo hivi hutukia kwenye mataifa ya Afrika na Asia.