Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama lilikutana asubuhi kuzingatia shughuli za Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Vita katika Yugoslavia ya Zamani (ICTY) na Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR). Mwendesha Mashitaka wa ICTY, Serge Brammertz kwenye taarifa aliowasilisha kwenye kikao hicho, alikumbusha 2009 ni mwaka wa mwisho wa Mahakama kuendeleza shughuli kamili kabla kuanza kupunguza watumishi wake katika 2010. Vile vile Hasan Jallow, Mwendesha Mashitaka wa ICTR ameliomba Baraza la Usalama kusaidia kuyahimiza mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kuwashika na kuwapeleka kwenye Mahakama ya ICTR wale watoro wanaotafutwa na waliotuhumiwa makosa ya jinai. Jallow alisema fungu kubwa la darzeni ya watuhumiwa hao hivi sasa wanaishi Kenya na katika JKK, mataifa ambayo serikali zao zinawajibika kuwashika na kuwahamisha kwenye Mahakama ya ICTR iliopo Arusha, Tanzania kukabili haki.

Ashraf Qazi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan amethibitisha kuwa UM unashiriki kwenye maandalizi ya mkutano ulioitishwa na Marekani, utakaojumuika Washington D.C. ili kufanya mapitio ya Mapatano ya Amani ya Jumla ya 2005 (CPA) kati ya Serikali ya Sudan na Sudan ya Kusini. Qazi ambaye anazuru Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini alisema UM unaisaidia Marekani kurahisisha shughuli za mkutano. Alikumbusha makundi yoooota ya wahusika waliotia sahihi Maafikiano ya CPA wanakabiliwa na masuala magumu kadha wa kadha kwenye juhudi zao za kukamilisha utekelezaji wao mwafaka huo kabla ya 2011.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay leo mjini Geneva alihutubia kikao cha 11 cha Baraza la Haki za Binadamu, ambacho kilifunguliwa rasmi Ijumanne. Kwenye risala yake alitilia mkazo umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha raia walionaswa kwenye mazingira ya mapigano huwa wanapatiwa hifadhi inayofaa. Aliangaza masuala yanayohusu hali ya fujo na vurugu iliotanda katika Afghanistan, Pakistan, Iraq, Colombia, Usomali, JKK na pia katika Sudan na Chad. Kuhusu hali katika Eneo Liliokaliwa Kimabavu la Falastina, alihimiza kupatiwa ushirikiano kamili katika kazi zake ile Tume ya Kuchunguza Ukweli juu ya mashambulizi yaliofanyika katika miezi ya karibuni, kwenye Tarafa ya Ghaza, kama ilivyoidhinisha Baraza la Haki za Binadamu. Juu ya mkutano wa mapitio ya mapendekezo ya Durban dhidi ya ubaguzi kimataifa, uliofanyika mwezi Aprili, alisema Waraka Halisi wa Matokeo ya Mkutano umethibitisha wazi kabisa, jukwaa jipya la kusukuma mbele utekelezaji wa Mwito wa Durban dhidi ya Ubaguzi Ulimwenguni.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limetoa mwito wenye kupendekeza kubuniwe mfumo mpya unaotakikana kuwapatia mahali pa hifadhi inayoridhisha, wale vijana wenye kuomba hifadhi za kisiasa katika nchi za Ulaya ya Kati, hasa wale vijana wenye umri kati ya miaka kumi na tatu mpaka ishirini. Mfumo huo mpya unatarajiwa kukidhi vyema mahitaji halisi ya vijana, na ni mradi mkubwa kabisa ambao haujawahi kutekelezwa hapo kabl na UNHCR. Shirika hili la wahamiaji linatumai jumuiya ya kimataifa itazingatia mapendekezo hayo na kuyatekeleza haraka iwezekanavyo.