Skip to main content

Nchi zinazotunza vinasaba vya mimea anuwai kufadhiliwa msaada wa fedha na taasisi ya kimataifa

Nchi zinazotunza vinasaba vya mimea anuwai kufadhiliwa msaada wa fedha na taasisi ya kimataifa

Mkutano wa Hadhi ya Juu wa wajumbe wa Bodi la Utawala la Taasisi ya Kutekeleza Mkataba wa Kimataifa Kutunza Rasilmali ya Vinasaba vya Mimea kwa Chakula na Kilimo, unaofanyika hivi sasa mjini Tunis, Tunisia umetangaza kuwa mataifa yanayoendelea 11 yanayotekeleza ile miradi ya kuhifadhi akiba ya mbegu za mimea kwa chakula na kutunza vinasaba vya mazao makuu, yatafadhiliwa msaada wa dola 500,000.

Msaada huu wa fedha utahudumia miradi ya kutunza vinasaba vya mbegu za mimea mikuu katika Misri, Kenya, Costa Rica, Bara Hindi na Peru, pamoja na Senegal, Uruguay, Nicaragua, Cuba, Tanzania na Morocco. Hii ni mara ya kwanza msaada kama huu hupatiwa mataifa husika, kwa kuambatana na mpango wa kuwasaidia kifedha wakulima wa nchi zinazoendelea, zenye kutunza akiba ya vinasaba vya mimea anuwai kwenye maeneo yao.