Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Uturuki umekabidhiwa uraisi wa duru wa Baraza la Usalama kwa mwezi Juni, baada ya Shirikisho la Urusi kukamilisha uongozi wa shughuli za Baraza kwa mwezi Mei. Wajumbe wa Baraza la Usalama watakutana Ijumanne asubuhi kuzingatia mpango wa kazi na ajenda ya mikutano ya mwezi Juni. Baada ya hapo, Balozi Baki Ilkin wa Uturuki atafanya mazungumzo na waandishi habari wa kimataifa wa Makao Makuu, kuelezea masuala yatakayopewa umuhimu kwenye mijadala ya Baraza la Usalama chini ya uongozi wa Uturuki.

Kwenye kikao kisichokuwa rasmi cha Baraza Kuu, kilichofanyika leo asubuhi, KM Ban Ki-moon aliwasilisha ripoti maalumu juu ya maendeleo kuhusu kazi za UM, ikijumlisha taarifa ya ziara alizofanya wiki za karibuni, nje ya Makao Makuu, na vile vile alizungumzia shughuli muhimu za UM katika wiki zijazo. KM alisema alipokuwa Geneva kuhudhuria Mkutano wa Kupunguza Silaha Duniani, alifanikiwa kuwahamasisha wajumbe wa kimataifa kufikia maafikiano ya mpango wa utendaji ulioshindwa kukamilishwa kwa muda wa miaka 12. Alitumai maafikiano haya yataashiria maendeleo ya kutia moyo kwenye kudhibiti uenezaji wa silaha za kinyuklia duniani. Lakini alisema pia alisikitishwa na uamuzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK) wa kung'ang'ania mtazamo unaopuza juhudi za kimataifa za kupunguza silaha. Alirudia mwito wake wa siku za nyuma ulioisihi DPRK kujizuia kuchukua hatua ziada tofauti, alizozitafsiri kama za uchokozi, na kuitaka serikali irejee kwenye yale mazungumzo ya kimataifa, ya upatanishi ya pande sita. Juu ya hali katika Sri Lanka, alisema KM hakuridhika kabisa na idadi kubwa ya vifo vya raia vilivyosababishwa na mapigano baina ya Serikali na kundi la wapinzani yalipamba nchinihumi majuzi. Serikali ya Sri Lanka iliombwa iuridhie mwito uliotolewa na jumuiya ya kimataifa, wa kubuni tume maalumu huru ya kuchunguza ukiukaji wa haki za kiutu - uliofanyika kwenye eneo la mapigano - kwa kupitia Baraza la Haki za Binadamu, Baraza Kuu na Baraza la Usalama la UM. Kuhusu mtafaruku uliolivaa taifa la Pakistan kwa sasa hivi, KM alikumbusha watu milioni 2.4 wamelazimika kuhajiri makazi kutoka eneo la bonde la Swat, na wanahitajia kusaidiwa kidharura na jumuiya ya kimataifa ili kunusuru maisha ya umma. KM alisema khumsi moja tu ilipokelewa kutoka wahisani wa kimataifa kuambatana na ombi liliopendekezwa na UM la kuchangishwa msaada wa dola milioni 543 kwa Pakistan, na inakhofiwa hali hiyo itailazimisha UM kupunguza baadhi ya huduma zake kwenye eneo la vurugu la Pakistan pindi itaendelea kunyimwa jumla iliosalia.

Meja Jenerali Mbutyana Duma Dumisani wa Afrika Kusini amewasili kwenye mji wa El Fasher mwisho wa wiki iliopita, kuchukua madaraka mapya ya Naibu Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID), baada Meja Jenerali Emmanuel Karenzi wa Rwanda kukamilisha muda wa kazi hivi karibuni. Dumisani alisema masuala yanayohusu maamirisho ya miundombinu na matatizo ya uenezaji wa majeshi kwenye maeneo ya mvutano ni masuala ambayo amenuia kuyapa muhimu wa dharura kwa sasa.

Julitta Onabanjo, Mjumbe Mkaazi wa UM katika Tanzania, alinakiliwa na Msemaji wa KM ya kuwa aliwaambia wageni waliohudhuria taadhima za Sikukuu ya Kumbukumbu za Walinzi Amani wa UM mjini Dar-es-Salaam majuzi, kwamba kundi la wahudumia amani 835 kutoka Tanzania, wanatazamiwa mnamo siku za karibuni kujiunga na vikosi vya UNAMID katika Darfur, ikijumlisha pia wanajeshi 22 wanawake.