Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Tume ya Kuchunguza Ukweli juu ya Vita katika Tarafa ya Ghaza, iliobuniwa rasmi mwezi uliopita kwenye kikao maalumu cha Baraza la Haki za Binadamu Geneva, inatarajiwa kuelekea Ghaza mnamo mwisho wa wiki hii, kwa kupitia kivuko cha Rafah, kiliopo upande wa Misri. Tume ya watu watatu, inayoongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini, itawasili Ghaza Juni mosi na itakutana na makundi husika yote na mgogoro wa eneo hilo, ikijumlisha mashirika yasio ya kiserikali, jumuiya za kiraia, mashirika ya UM, waathirika wa mashambulio ya Israel pamoja na kuklutana na wale mashahidi wengine wanaohusika na madai ya kufanyika ukiukaji wa haki za kibinadamu katika eneo liliokaliwa. Tume ya Barazala Haki za Binadamu pia itakutana na watu wengine wenye taarifa ziada juu ya ukweli wa matukio yanayofanyiwa uchunguzi katika Ghaza.

Ijumaa asubuhi wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa Kupunguza Silaha Duniani Geneva, walipitisha warka maalumu wa makubaliano kuhusu ratiba ya mpango wa kazi kwa Mkutano wa 2009, ratiba ambayo ilikwamishwa na kuzusha siutafahamu miongoni mataifa kwa karibu miaka kumi na mbili. Uamuzi wa mkutano wenye rakamu ya CD/1863, ulitilia mkazo umuhimu wa kuwa na wahusika wengi wa kimataifa wenye kuzingatia na kujadilia masuala ya kupunguza silaha ulimwenguni, na umependekeza kuundwe Makundi ya Kufanya Kazi na kuchaguliwa Waratibu Maalumu wa kusimamia kadhia za Mkutano. Kikao cha wawakilishi wote cha Mkutano, kitachoongozwa kwa mara ya kwanza na Argentina, kitafanyika Alkhamisi ijayo, tarehe 04 Juni 2009.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwamba sasa hivi walimwengu wanashuhudia moja ya uhamisho wa kasi, kihistoria, usio kifani, wa raia wanaong'olewa makazi katika Pakistan, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa muda wa miaka 15. Mapigano baina ya vikosi vya serikali ya Pakistan na majeshi ya mgambo ya wapinzani wenye siasa kali, kwenye Jimbo la Mpakani la Kaskazini Magharibi (NWFP) yamechochea watu karibu milioni 3 kung'olewa makazi, na inafikiriwa kitendo hiki kuwa ni uhamisho mkubwa kabisa wa raia katika Pakistan tangu taifa hilo kubuniwa. Kwa mujibu wa OCHA, watu waliosalia kwenye eneo la mapigano la NWFP sasa hivi, wanakabiliwa na hatari kubwa kimaisha. Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa upande wake, limeonya watu waliohamishwa makazi kimabavu kutoka NWFP wanakabiliwa na hatari ya miripuko ya maradhi ya kuambukiza kwenye kambi za wahamiaji za makazi ya dharura. Mashirika ya UM juu ya Wahamiaji, UNHCR, na makazi, UN-HABITAT, yameripotiwa kuongeza shughuli zao za kuwahudumia kihali wale waathirika waliong'olewa makazi ambao wameamua kukaa na aila za kienyeji, ambazo zimeshuhudia muongezeko mardufu wa wakazi kwenye kaya zao.

Ripoti mpya ya KM juu ya shughuli za Ofisi ya Huduma Mchanganyiko za Ujenzi wa Amani katika Sierra Leone iliowasilishwa wiki hii, imebainisha kufufuka tena karibuni fujo na vurugu za kisiasa nchini. Ripoti ilipongeza Serikali ya Sierra Leone kwa kuchukua hatua ya kutobisha fujo hiyo kwa vitendo ambavyo vingelitekelezwa, vingelianzisha tena duru hatari, na ovu, ya mashambulio na mapigo ya kujibizana. Kwa mwelekeo huo wa Serikali, ripoti ya KM ilitilia mkazo, viongozi na raia wa kawaida katika Sierra Leone wameonyesha mfano na matumaini ya kutia moyo kuhusu utulivu wa taifa lao kwa maisha ya wakati wa baadaye, na kuonyesha mfano mzuri wa kufuatwa vile vile na mataifa jirani ya kikanda. Wakati huo huo KM ametoa ombi kwa wahisani wakimataifa kutopwelewa kuchangisha misaada ya kuhudumia ujenzi wa amani katika Sierra Leone, licha ya kuwa walimwengu tunakabiliwa na mizozo ya kifedha katika soko la kimataifa.

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) limeripoti Ijumaa ya leo kuhusu mataifa ya Afrika kufikia tukio la kihistoria, kwenye zile huduma za kupambana na taathira za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Mawaziri wa Mazingira wanaowakilisha mataifa 30 ziada ya Afrika wamepitisha Mwito wa Nairobi, unaohusu maafikiano yatakayowasaidia kuwa na jukwaa halisi la kujitetea kwa uzito zaidi, juu ya dharura ya kufadhiliwa misaada ziada ili kujikimu kimazingira, kwenye Mkutano wa Copenhagen kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa, utakaofanyika rasmi mwezi Disemba. UNEP pia imeripoti ya kwamba kuanzia tarehe 01 Juni 2009 wajumbe 3,000 wenye kuwakilisha serikali, wafanyabiashara, mashirika yanayopigania hifadhi ya mazingira na taasisi za utafiti watakusanyika Bonn, Ujerumani kwenye duru mpya ya mazungumzo yatakayojadilia waraka wa kuzingatia suluhu ya pamoja kwenye udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hewa duniani.