Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Taasisi ya Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) yamehadharisha ya kuwa mtindo wa wageni kumiliki ardhi za kizalendo - hususan katika bara la Afrika - ni tatizo linaloashiria wazalendo maskini huenda wakafukuzwa kutoka maeneo haya au kunyimwa uwezo wa kumiliki mali hiyo kuendesha maisha. Mashirika ya FAO na IFAD yameyahimiza Mataifa Wanachama kuhakikisha sheria za kumiliki ardhi kwa jamii zinazoishi kwenye vijiji zinahishimiwa, na kuwahusisha wenyeji hawa kwenye makubaliano yote yanayohusu biasahara ya kuwauzia wageni ardhi katika siku za baadaye .

 Hii leo kwenye mji wa Geneva, Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu limeanzisha kikao maalumu kuzingatia hali ya haki za kiutu katika Sri Lanka, kufuatia mapigano ya karibuni kisiwani humo. Kwenye ujumbe alioutuma mkutanoni, kwa kupitia njia ya vidio, Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu alibainisha kupokea hoja zenye ushahidi mzito, uliothibitisha pande zote mbili za kwenye mapigano ya karibuni Sri Lanka, ziliharimisha, kwa udhahiri mkubwa, kanuni za msingi dhidi ya haki zisiokiukwa za raia. Aliusema kunahitajika kuundwe tume ya kimataifa, ilio huru na inayoaminika, kufanya uchunguzi juu ya matukio ya karibuni dhidi ya raia kwenye eneo la mapigano Sri Lanka, ili kutafuta ukweli kuhusu baadhi ya matukio yalioharimisha kihorera, na kukiuka sheria za kiutu za kimataifa na haki za binadamu dhidi ya raia.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeeleza kwamba maelfu ya WaPakistani wanaendelea kuhajiri eneo la mgogoro, katika Jimbo la Mpakani la Kaskazini Magharibi (NWFP), ambapo vikosi vya serikali vinaripotiwa kushiriki kwenye mapigano na wapambanaji wazalendo wenye siasa kali. Jumla ya watu waliosajiliwa kuhama makazi, kwa ujumla, kuanzia mwanzo wa Mei hadi sasa, kwa sababu ya mapigano, imefikia milioni 2.38 ziada. UNHCR inakadiria wahajiri 126,000 husajiliwa kila siku kwenye wilaya nne za Mardan, Charsadda, Swabi na Nowshera. Kadhalika, imeripotiwa raia wingi wengineo bado wamenaswa kwenye maeneo ya mgogoro. Wakati huo huo, UNHCR imepongeza ukarimu mkubwa ulionyeshwa na raia wa kawaida katika Pakistan waliojitolea kubeba majukumu ya kuwahudumia misaada ya kihali, na kwa khiyari, wazalendo wenziwao kwa kuwapatia, mathalan, vifurushi vya chakula vinavyojumuisha unga wa ngano, sukari, viungo vya kupikia, chai na hata fedha za matumizi na nguo. Sasa hivi UNHCR inajaribu kununua vifaa vya kuhudumia wahamiaji katika Pakistan, badala ya kuagizishia nje, ili kurahisisha ugawaji wa misaada ya kihali kwa umma muhitaji. Vile vile UNHCR inapeleka Pakistan misaada ziada ya kihali, pamoja na bidhaa na vifaa kutoka maghala ya UM yaliozagaa sehemu kadha wa kadha za dunia. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kwa upande wake limehadharisha watu zaidi watalazimika kuyahama makazi katika siku za karibuni, pale operesheni za jeshi la Pakistan zitakapopanuliwa kwenye maeneo mapya ya mapigano.

Asubuhi Baraza la Usalama limepitisha azimio 1872 (2009) juu ya hali katika Usomali, azimio ambalo lilishtumu kufufuka tena kwa mapigano nchini humo katika wiki za karibuni, na kuttaka uhasama usisitishwe haraka iwezekanavyo. Azimio lilipitishwa bila upinzani na wajumbe wote 15 wa Baraza la Usalama. Kadhalika azimio limeidhinisha muda wa shughuli za vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika katika Usomali vya AMISOM uongezwe mpaka tarehe 31 Januari 2010. Vile vile Baraza la Usalama limeyataka makundi yanayohasimiana Usomali yatekeleze Mapatano ya Djibouti. Baada ya hapo Baraza la Usalama lilijadilia ripoti za Kamati ya Kupambana na Ugaidi unaoambatana na makundi ya Al-Qaida na Taliban. Baraza pia lilisikiliza ripoti za Kamati inayoshughulikia udhibiti wa silaha za maangamizi.

Helen Clark, Mkuu mpya wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) alipowasilisha risala yake ya awali, tangu kuanza kazi, mbele ya wajumbe wa bodi la utendaji la shirika alikumbusha kwamba uzoefu wa kazi unaambatana na mazingira ya kuleta haki kwenye shughuli zote za uchumi na jamii kwa natija ya umma. Alisema katika kipindi tuliomo sasa hivi kimataifa tumebahatika kujaaliwa mali maridhawa, taaluma na pia teknolojiya marudufu zenye uwezo hakika wa kuimarisha maisha duni ya watu maskini na umma dhaifu kote ulimwenguni. Kilichokosekana, alitilia mkazo, ni hamasa ya kisiasa ya kutekeleza miradi na huduma zinazohitajika kuyafikia malengo hayo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Kimataifa juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) yameanzisha Mradi wa Pamoja Kudhibiti Saratani, wenye lengo la kuimarisha na kuharakisha juhudi za kupambana na maradhi ya saratani katika mataifa yanayoendelea.