Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Tarehe 25 Mei huadhimishwa kila mwaka na UM kuwa ni Siku ya Afrika. Kwenye risala ya KM kuiadhimisha siku hii, alisisitiza kwamba UM utaendelea kuzitekeleza zile ahadi ilizotoa hapo kabla za kuusaidia umma wa Afrika, kwa ujumla, kwenye kadhia muhimu za kudumisha amani, usalama na maendeleo yanayosarifika ya kiuchumi na jamii. Siku ya Afrika inaadhimishwa kwa kuambatana na ile tarehe rasmi ya ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) katika 1963, taasisi ambayo sasa hivi hutambuliwa kama Umoja wa Afrika (UA). Siku ya Afrika huangaza mafanikio yaliodhihirika barani humo na pia kutathminia namna ya kukabiliana na masuala yaliosalia yenye kuhitajia mchango wa pamoja kuyasuluhisha kwa ushirikiano na wadau wa kimataifa.

 Baraza la Usalama lilitarajiwa kukutana jioni, kwenye kikao cha dharura, kujadilia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea/Korea Kaskazini (DPRK), taifa ambalo linaripotiwa Ijumatatu liliripua chini ya ardhi bomu la majaribio la kinyuklia. Majadiliano haya yataongozwa na Urusi, taifa lilioshika wadhifa wa uraisi wa Baraza kwa mwezi Mei. Kufuatia madai ya kuwa DPRK iliendesha majaribio ya bomu la nyuklia katika Oktoba 2006, wajumbe 15 wa Baraza la Usalama walitoa mwito wa kuisihi DPRK "kutofanya majaribio ziada ya silaha za kiatomiki, na pia kuitaka isirushe, kwa majaribio, makombora ya masafa marefu". Baraza lilipendekeza vikwazo fulani viwekewe Korea ya Kaskazini. Hata hivyo, katika siku za karibuni, DPRK iliamua kurusha kombora la masafa marefu, licha ya upinzani mkubwa kutoka KM wa UM, Ban Ki-moon pamoja na jumuiya ya kimataifa, ambao walipendekeza pamoja kufufua haraka yale mazungumzo ya Pande Sita, yakijumuisha DPRK, Jamhuri ya Korea (Korea ya Kusini), Ujapani, Uchina, Urusi na Marekani, ili kusuluhisha mzozo huu kwa amani.

Ripoti iliotolewa na Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) hii leo imeshtumu mapigano makali yaliofumka Ijumapili, ndani na karibu ya mji wa Umm Baru, kilomita 100 kutoka mpaka na Chad, katika magharibi ya mbali ya jimbo la Darfur Kaskazini. Mapigano haya, yaliochukua saa kadha, yaliendelezwa baina ya vikosi vya Serikali ya Sudan na kundi la waasi la JEM. Kadhalika, ripoti imeleza Ijumapili usiku kulisikika miripuko mbalimbali muda tu baada ya ndege za Serikali kuonekana zikiruka kwenye eneo hilo. Kwa mujibu wa ripoti, watu 53 walijeruhiwa vibaya kutokana na mapigano, ikijumlisha raia, wanajeshi wa Serikali na wafuasi wa waasi wa JEM.