Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould Abdallah, ametangaza kuwa kuna dalili za kutia moyo kwamba wale raia 45,000 waliouhama mji wa Mogadishu katika siku za karibuni, kwa sababu ya kukithiri kwa mapigano, huenda wakarejea makwao katika muda mchache ujao. Aliiambia Redio ya UM kwamba fununu hii inaambatana na taarifa alizopokea zenye kuonyesha vikosi vinavyounga mkono serikali, ambavyo vilianzisha mashambulizi mapya ya kukabiliana na wapiganaji aliowatafsiri kama wafuasi WaIslam wenye siasa kali, huenda wakaudhibiti mji karibuni.

Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) limetoa ripoti mpya ya mwaka, kuhusu hali ya afya, kijumla, kwa wakazi wa  Tarafa ya Ghaza, hali ambayo inaendelea kuharibika kwa sababu ya vikwazo vilioekewa na wenye mamlka Israel. UNRWA iliripoti vile vile kwamba haikufanikiwa kuvitengeneza vile vituo vya afya vya Ghaza vilivyobomolewa na mashambulio ya vikosi vya Israel kwenye mapigano ya mwanzo wa mwaka. Ililaumu ya kuwa upungkufu wa karatasi umesambaratisha huduma za kuhifadhi ripoti za afya ya mgonjwa kwenye madaftari. Kwa wakati huo huo UNRWA imeeleza bajeti lake la kuhudumia afya kwa sawa ni dola milioni 80, za kutumiwa kwa watu milioni 4, ikimaanisha UNRWA itatumia dola 20 tu kwa mwaka kukidhi mahitaji ya afya kw akila mtu. Kwa kulingana na bayana hii UNRWA imesema imelazimika kufunga baadhi ya hospitali kutokana upungufu wa fedha za kuhudumia afya, ikijumlisha hospitali ya Qalqilya iliopo katika Magharibi ya Mto Jordan; na UNRWA imelazimika pia kupunguza huduma nyengine za afya.

KM Ban Ki-moon amewasili Sri Lanka, leo Ijumaa, kufanya ziara maalumu yenye malengo matatu: kufarajia haraka misaada ya kiutu kwa waathirika wa mapigano yaliopamba nchini humo majuzi; kuhakikisha jamii husika zitasaidiwa kurejea, kwa usalama, kwenye maisha ya kawaida na pia kujengewa makazi mapya; na KM atajaribu pia kuwasilisha suluhu ya kisiasa inayosarifika na yenye usawa kwa raia wote. Saa chache kabla ya hapo, Vijay Nambiar, Mnadhimu Mkuu katika Ofisi ya KM alikutana na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Colombo ambapo alidhihirisha ya kuwa UM una matumaini makubwa ziara ya KM "itasaidia kuhamasisha ufufuaji wa shughuli za kiuchumi na jamii kineo, na kuleta upatanishi unaoridhisha miongoni mwa Sri Lanka wote."

Juu ya hali katika Pakistan, KM ametoa taarifa yenye kuisihi jumuiya ya kimataifa kuonyesha ushikamano wa kuridhisha na umma wa Pakistan, kwa kujumuisha michango maridhawa kwenye Mradi wa Kufadhilia Misaada ya Kiutu ulioanzishwa rasmi Ijumaa kwenye mji wa Islamabad, pamoja na kusaidia ule Mpango wa Ujenzi Mpya na Ufufuaji wa Uchumi na Huduma za Jamii uliowasilishwa juzi na Serikali ya Pakistan. KM alisema ana wasiwasi juu ya mfumko wa kasi wa watu waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano, na kutilia mkazo kwamba misaada inayofadhiliwa waathirika wa hali hiyo, kwa ushirikiano na Serikali ya Pakistan na mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu, ndio yenye ufunguo halisi wa kukidhi mahitaji ya msingi kwa watu milioni 1.7 waliong'olewa makazi.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) katika Pakistan limeripoti kuwa linashiriki kwenye shughuli za kuwapatia vifaa vya makazi ya muda raia waliong'olewa makazi na kuwapatia hifadhi kinga dhidi ya joto kali liliopamba huko, hali ambayo katika majira ya sasa hufikia digrii 45 ya kipimo cha selsiasi (45'C). Shirika la UM Linalohusika na Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) nalo kwa upande wake limetangaza mama wajawazito 70,000 waliong'olewa mastakimu katika Bonde la Swat wanahitajia kupatiwa uangalizi na utunzaji wa dharura wa afya, hali ambayo, ilihadharisha, huenda ikaharibika zaidi kwa sababu ya ukosefu wa matunzo. Wajawazito vile vile wanahitajia uangalizi wa kabla kuzaa, na misaada ya uzazi pamoja na matunzo ya uzazi wa dharura. Wanawake wenye mimba 6,000 wanatazamiwa kuzaa mnamo mwezi ujao, na fungu kubwa la wajawazito hawa watahitajia kupasuliwa ili kudhibiti matatizo yanayofungamana na uzazi.