UNDP na UNAIDS washirikiana na wabunge wa Afrika na Mashariki ya Kati kupambana na UKIMWI

UNDP na UNAIDS washirikiana na wabunge wa Afrika na Mashariki ya Kati kupambana na UKIMWI

Karibuni kulianzishwa ushirikiano mpya baina ya mashirika ya UM na taasisi ya wabunge wa kutoka Afrika na Nchi za Kiarabu, kwa makusudio ya kujumuisha jitihadi zao kwenye kadhia ya kudhibiti bora maambukizi ya vimelea vya UKIMWI kwenye maeneo yao.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limeripoti kwamba majuzi wajumbe wanachama wa Baraza la Wabunge wa Nchi za Kiarabu na Kiafrika juu ya Maendeleo na Udhibiti wa Idadi ya Watu  (FAAPPD), wakichanganyika na maofisa wa Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) pamoja na wale wanaowakilisha Shirika la Miradi ya Maendeleo (UNDP) katika Afrika ya Kati na Magharibi , walitiliana sahihi, taarifa ya maafikiano maalumu, yalioahidi kushirikiana, kwa pamoja, kwenye zile huduma za kuwapatia raia zao, uwezo wa kufikia na kupokea taarifa kinga dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, na pia kuhakikisha kuwapatia fursa za matibabu, uangalizi na uuguzi wa maradhi unaofaa kwa wale watu waliopatwa nayo.  Kwa mujibu wa takwimu za UM, katika 2007, watu milioni 5 ziada katika Afrika ya Kati na Afrika Magharibi walithibitika kuishi na vimelea vya UKIMWI . Kwa mfano, katika Nigeria, taifa la pili liliopo kusini ya Jangwa la Sahara lenye idadi kubwa ya wenye virusi vya UKIMWI, imeripoti wagonjwa milioni mbili walioambukizwa na virusi vya UKIMWI kwenye nchi.

Katika mwaka 2006, Mataifa Wanachama kwenye UM yaliahidi ya kuwa yatajitahidi kufanya kila yawezalo kuhakikisha umma wa kimataifa utapatiwa uwezo wa kupokea taarifa kinga, halali, dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI, pamoja na kuchangisha fedha zinazohitajika kutekeleza miradi kama hiyo, kwa kulinganana uwezo walionao ili kumudu kadhia hii. Lakini nchi nyingi za Afrika, hasa zile ziliopo kusini ya Jangwa la Sahara, hazina uwezo wa fedha za kugharamia huduma za mawasiliano ya jamii, zinazohitajika kuukinga umma na mambukizi ya virusi vya UKIMWI. Mataifa haya yamenyimwa misaada ya kuridhisha kumudu huduma hizo kwa sababu kadha wa kadha, kama vile vurugu na fujo zilizotanda kwenye maeneo yao, ubaguzi dhidi ya wagonjwa wa UKIMWI, ikichanganyika na mapuuza pamoja na fedheha zinazowatenga wagonjwa wa UKIMWI kupata taarifa kinga za afya , na vitendo vyenginevyo kama hivi ambavyo hukiuka haki za binadamu.

Kwa hivyo, maafikiano yaliotiwa sahihi na taasisi ya baraza la wabunge wa nchi za Kiarabu na Kiafrika, wakichanganyika na mashirika ya UM ya UNDP na UNAIDS yanaashiria matumaini ya kutia moyo katika kupambana na UKIMWI kwenye maeneo husika. Maafikiano haya yatawapatia wabunge fursa ya kutumia nyadhifa zao kuamsha hisia na maoni ya jamii, kwa ujumla, juu ya umuhimu wa kujikinga na maambukizi maututi ya UKIMWI. Kadhalika, wabunge hawa ilivyokuwa ndio wenye dhamana ya kutunga sheria za kitaifa, wana fursa pia ya kuandaa kanuni maalumu zitakazosaidia vile vile kutunza na kuhifadhi haki za kiutu za wagonjwa wa vimelea vya UKIMWI kitaifa, kwa kuhakikisha sheria hizo zitahishimiwa na, hatimaye, kuwaokoa wale raia wagonjwa, walio dhaifu kihali na mali, dhidi ya usumbufu na kashfa zinazotokana na kutengwa na jamii zao. Halkadhalika, wabunge husika, kwa sababu ya maafikiano yao, wataweza kutumia vyeo walivyo navyo kuhimiza serikali zao kuweka kando posho fulani la bajeti la taifa, fedha amabzao zitatumika kukabiliana na UKIMWI, na kwa wakati huo huo kufuatilia matumizi ya msaada huu katika kukidhi mahitaji ya watu wenye kuishi na vimelea vya UKIMWI.

Baraza la Wabunge wa Nchi za Kiarabu na Kiafrika juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu na Maendeleo (FAAPPD) lilianzishwa rasmi 1997, na linajumlisha wajumbe wabunge kutoka nchi 61 za Afrika kusini ya Sahara na kutoka maeneo ya Mashariki ya Kati.