Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Staffan de Mistura, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Iraq ameshtumu, kwa kauli kali, mashambulio ya mabomu yaliotukia Kirkuk leo Alkhamisi na yale mashambulio mengine yaliofanyika kwenye mji wa Baghdad hapo jana. De Mistura alisema vitendo hivi viliwakilisha "uhalifu uliolenga kihorera raia wa Iraq" na vikijumuisha "jinai ya kulaumiwa vikali" na jamii yote ya kimataifa. Mjumbe wa KM kwa Iraq aliwatumia, kwa masikitiko makubwa aila za wafiwa, mkono wa taazia, kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na vile vile aliwaombea waathiriwa majeruhi wapone haraka.

Shirika la UM Linalosimamia Amani Cote d'Ivoire (UNOCI) limetoa mwito unaopendekeza kuanzishwe haraka zile shughuli za kuandikisha wapiga kura nchini kwa uchaguzi ujao. UNOCI imetaka taasisi zote husika na kadhia hii, pamoja na wenye mamlaka katika Cote d'Ivoire, wakichanganyika na vyama vya kisiasa, na ikijumlisha Kamisheni Huru ya Uchaguzi, kuhishimu ile siku iliokubaliwa na wote kufanyisha uchaguzi, yaani siku ya tarehe 29 Novemba 2009. Kwa hivyo, kwa kulingana na pendekezo hili, UNOCI imeyakumbusha makundi husika yote juu ya umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa majukumu yaliosalia ya uchaguzi, na kuhakikisha uchaguzi utakapofanyika karibu namwisho wa mwaka utakuwa huru, wenye uwazi na wa haki kwa wote.

UM unaiadhimisha tarehe ya leo kuwa ni Siku ya Tamaduni Anuwai Kukuza Maendeleo na Mawasiliano. Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeihishimu siku hii kwa kuhamasisha nchi zote ulimwenguni kujitahidi kutunza, na kuimarisha tamaduni anuwai, na zilizo tofauti kimataifa. UNESCO, kwa upande wake, iliandaa sherehe na tamasha mbalimbali za kimataifa za siku tisa, ambazo zitafikia kilele kesho Ijumaa kwenye mji wa Paris, Ufaransa, palipo makao makuu yake.

Mnamo asubuhi ya Ijumatano, ya tarehe 20/05/2009, kwenye Ukumbi wa Mikutano ya Baraza la UM juu ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) walikusanyika wawakilishi wa kimataifa kwenye taadhima maalumu, ya kumuidhinisha Russel Simmons kuwa Balozi Mfadhili juu ya Kumbukumbu ya Kudumu ya UM iliokusudiwa kuwaheshimu waathiriwa wa Biashara ya Watumwa kati ya Maeneo ya Ng'ambo ya Bahari ya Atlantiki, kumbukumbu ambayo inatazamiwa kukamilishwa kutengenezwa 2012. Simmons ni mtu mashuhuri kwenye ulimwengu wa wasanii, na anajulikana duniani kote kuwa ni mwasisi wa ule mtindo wa muziki unaotmabuliwa kama ‘hip-hop'. Taadhima hizi zilizofanyika katika Makao Makuu ya UM kwenye jiji la New York, vile vile zilitumiwa kuanzisha Mfuko wa Amana kufadhilia Kumbukumbu ya Kudumu ya UM ya kuhishimu waathirika wa utumwa. Maofisa Wakuu wa UM, Wawakilishi wa Kudumu kutoka Mataifa Wanachama pamoja na wale kutoka jumuiya ya wanadiplomasiya na waandishi habari wa kimataifa walijumuika pamoja kwenye taadhima hii. Kundi la mataifa ya Karibiani, yakiungwa mkono na wanachama wa Umoja wa Afrika ndio walioandaa na kutayarisha taadhima za kuanzisha kuchangisha fedha za kuhudumia Kumbukumbu ya Kudumu ya UM kwa Wathirika wa Utumwa.