Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa WHO anasema taarifa inayoaminika ya H1N1 ni muhimu kutuliza wahka wa umma kimataifa

Mkuu wa WHO anasema taarifa inayoaminika ya H1N1 ni muhimu kutuliza wahka wa umma kimataifa

Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la WHO, kwenye mashauriano ya kiwango cha juu kuhusu maambukizi ya homa ya mafua ya A(H1N1) yaliofanyika Geneva Ijumatatu, alitilia mkazo umuhimu wa kuripoti "taarifa halisi za kitaaluma, zinazoaminika, juu ya vipengele mbalimbali vilivyodhihiri kuhusu ugonjwa huu, na kuwawezesha wataalamu kufanya maamuzi ya dharura ya kudhibiti bora mfumko wa maradhi kwa kujitayarisha kukabiliana na janga hilo kimataifa."

Alihadharisha kwamba jumuiya ya kimataifa "imeelemewa na majukumu mazito yenye kushinikiza kuwepo maamuzi ya haraka ambayo yakitekelezwa huashiria athari za muda mrefu, kwenye mazingira yaliojaa wahka na wasiwasi mkubwa wa kisayansi." Alisema ni muhimu "kuziongoza nadharia na tabia za umma wa kimataifa, kwa kuwapatia taarifa za kisayansi juu ya mifumko ya maradhi hatari ya maambukizi" zitakazowasaidia kujikinga kama inavyotakikana na maambukizi ya kasi ya maradhi. Alitilia mkazo kwamba WHO inawajibika "kutoa hadhari za jumla kwa umma juu ya maradhi, pakihitajika, na kwa wakati huo huo kuwaondolea mashaka na kuwatuliza kwa taarifa zinazoaminika, ikiwezekana", taarifa ambazo zitabainisha kihakika hali halisi ya maradhi ilivyo. Alisema Dktr Chan msimamo kama huu ni "mgumu kuisawazisha,"na likumbusha vimelea vya homa ya mafua ya H1N1, kikawaida, vina uwezo mkubwa wa kutushangaza kwa miripuko ya ghafla. Hata hivyo, alitilia mkazo Dktr Chan, vimelea hivyo vya homa havikujaaliwa werevu walionao wanadamu. Kwa hivyo, alihimiza ushirikiano miongoni mwa sekta zote za kiserikali na jamii, pamoja na wadau muhimu wengineo, utakaosaidia kwenye zile juhudi za kuisuluhisha mizozo ya dharura ya afya ya jamii. Ripoti za Ijumatatu za WHO kuhusu maambukizi ya homa ya mafua ya A (H1N1) zimeonyesha nchi 40 duniani zimegundua jumla ya wagonjwa 8,829 walioambukizwa na virusi vya homa iliosababisha vifo 74. Licha ya bayana hii, WHO imesisitiza kwamba hakuna haja kwa hivi sasa ya kubadilisha kipimo cha tahadhari ya maambukizi, kipimo ambacho kitaendelea kusalia kwenye kiwango cha tano, cha ule mfumo wa viwango sita. Kiwango cha sita kikiripotiwa itamaanisha walimwengu wanakabiliwa na hatari kuu ya maambukizi ya janga la maradhi kimataifa.