Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon aliwaambia waandishi habari wa kimataifa Geneva ya kuwa atazuru Sri Lankia kuanzia tarehe 22 mpaka 24 Mei, ziara ambayo alisema imekusudiwa kuitika mwito wa dharura, kutoka jamii ya kimataifa, utakaosaidia “kutibu majeraha ya vita, yaliowatenga jamii zinazoishi Kisiwani humo kwa muda wa miongo mitatu.” Alisema kuwa ziara yake italenga zaidi zile sehemu zilizoathirika sana na mapigano ili kushuhudia, binafsi, hali ilivyo na kukadiria mahitaji ya waathirika wa vurugu.

Ujumbe wa Baraza la Usalama unaozuru Afrika Ijumanne umehitimisha ziara yao katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), baada ya kufanyisha mazungumzo, ya hadhi ya juu, kwenye mji mkuu wa Kinshasa, na wakuu wa serikali pamoja na Raisi Joseph Kabila na baadhi ya mawaziri muhimu. Mazungumzo yao yalizingatia masuala yanayohusu hali ya usalama katika JKK, mageuzi kwenye sekta ya ulinzi, juhudi za upatanishi baina ya JKK na Rwanda, na vile vile awamu ijayo kuhusu operesheni za Shirika la UM la Ulinzi Amani katika JKK (MONUC). Kwenye kikao kingine, wajumbe wa Baraza la Usalama walikutana na wabunge na walizungumzia haki za binadamu, mahitaji ya kuimarisha vyombo vya utawala kote nchini, na pia kusailia mfumo wa siasa wa kitaifa, ikijumuisha kanuni za uchaguzi. Baada ya hapo ujumbe wa Baraza la Usalama ulielekea Liberia, ambapo wanatarajiwa kukutana, kwa mazungumzo, na Raisi Ellen Johnson Sirleaf pamoja na wawakilishi wa serikali na maofisa wakaazi wa UM waliopo Liberia.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kununua, kwa mara ya kwanza, chakula kutoka wakulima wadogo wadogo katika Kenya, kwa kuambatana na ule mradi mpya wa kukuza kilimo unaojulikana kama ‘Ununuzi wa Kukuza Maendeleo' - au Mradi wa P4P, ambao huwapatia wakulima wenye pato dogo fursa ya kuuza bidhaa zao katika soko la kizalendo. Hatua hii inamaanisha WFP imewania kutekeleza sera mpya ya kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, kadhia ambayo itawapatia fursa ya kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa chakula na kuongeza akiba ya chakula ili kutumiwa siku zijazo wakati wa shida.