Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti kinga ya WHO dhidi ya maambukizi ya homa ya A(H1N1)

Ripoti kinga ya WHO dhidi ya maambukizi ya homa ya A(H1N1)

Alkhamisi (14 Mei 2009), taarifa ya Shirika la Afya Duniani juu ya hali ya maambukizi ya vimelea vya homa ya mafua ya H1N1 ulimwenguni ilieleza ya kuwa nchi wanachama 33 ziliripoti rasmi kwa WHO kugundua wagonjwa waliopatwa na maradhi hayo kwenye maeneo yao.

Jumla ya wagonjwa waliosajiliwa kimataifa, mnamo saa 06:00 za majira ya GMT ilikuwa 6497, ikijumlisha pia vifo 65. Wingi wa wagonjwa wa homa hii ya mafua wako Mexico na Marekani. WHO iliripoti wagonjwa 2446 waliambukizwa na vimelea vya homa ya H1N1 katika Mexico, homa iliosababisha pia vifo 60 nchini humo. Kadhalika, Marekani pia imethibitisha kugundua idadi kubwa ya watu waliopatwa na homa ya mafua ya H1N1, sawa na wagonjwa 3352, ikjumlisha pia vifo vitatu. Ugonjwa huu wa mafua ya H1N1 ni ugonjwa wa aina gani? Tutajaribu kuelimisha wasikilizaji wetu juu ya maradhi haya - tunaanza na suala lifuatalo:

SUALA: Vipi watu huambukizwa na homa ya mafua ya A(H1N1)?

AWK: Mripuko wa homa hii miongoni mwa wanadamu, kwa sasa hivi, hutokana na uambukizaji wa mwanadamu mmoja kwa mwanadamu mwengine. Watu walioambukizwa vimelea vya homa ya H1N1 wakikohoa, au wakipiga chafya, vitone vya vijidudu vya maradhi hutawanyika kwenye mikono yao, au huanguka kwenye sehemu ya juu ya kitu, sakafu au ukuta, na pia hutawannyika hewani. Mtu mwengine huweza kuambukizwa homa ya H1N1 kwa kuvuta hewa yenye vimelea vya maradhi, au kugusa zile sehemu zilizoathirika na vijidudu vya maradhi haya. Kuzuia vimelea vya homa ya mafua visitawanyike, watu wanawajibika kufunika midomo yao na pua kwa vitambaa au tishu pale wanapokohoa; na wakumbuke kuwa wanatakiwa waoshe mikono mara kwa mara, kwa maji safi, ili kujikinga na maambukizo yamaradhi.

SUALA: Dalili zipi au ishara gani huthibitisha kuwa mtu amepatwa au ameambukizwa na homa ya mafua ya H1N1?

AWK: Dalili za awali za maambukizi ya homa ya mafua ya A(H1N1) kwa mwanadamu ni kama zile za homa ya kawaida ya mafua; yaani mtu hujihisi na homa, hukohoa na kuumwa na kichwa, musuli na hupata maumivu ya maungo yote, pamoja na maumivu kwenye koo na kilimi. Mgonjwa pia hujikuta anatiririka mafua ovyo, na wakati mwengine huwa anatapikiana na kuharisha.

SUALA: Kuhusu utafiti wa mripuko wa awali wa maradhi haya, timu ya wataalamu wa WHO iliopelekwa Mexico kuchunguza chanzo cha homa ya mafua ya H1N1, wameripoti taarifa yoyote iliothibitisha kihakika kiini cha homa ya mafua na vipi ilisambazwa na kadhalika?

AWK: Timu kadha za wataalamu wa kimataifa bado zinaendelea kuitumia WHO matukio kadha ya uchunguzi wao juu ya kiini cha mripuko wa maradhi, na tutawakilisha jawabu sahihi nahalisi katika siku za karibuni.

SUALA: Kuna ithibati yoyote kwamba wanadamu waliambukizwa na vimelea vya homa ya mafua ya H1N1 kutoka nguruwe?

AWK: HAPANA.

SUALA: Kadhalika, UM una taarifa za aina gani zinazoelezea athari za kiuchumi kutokana na mripuko wa homa ya mafua?

AWK: HAKUNA TAARIFA JUU YA HALI HIYO.

SUALA: Basi kwa nini umma wa kimataifa umejaa wasiwasi na wahka juu ya kuenea kihorera ulimwenguni kwa homa ya mafua ya H1N1, hasa tukizingatia ya kwamba maelfu ya watu hufariki dunia kila mwaka kutokana na maradhi mengine ya mripuko ya misimu au majira?

AWK; Miripuko ya maradhi mengine yanayotukia mara kwa mara, kwa kulingana na majira au misimu ya kila mwaka, hali hiyo inaweza kudhibitiwa na WHO kwa sababu ya kuwana uzoefu wamuda mrefu katika kukabiliana na maradhi ya msimu, ambayo hutibiwa na chanjo maalumu za kimajira. Lakini mripuko wa janga la maradhi mapya, kama hii homa ya mafua ya H1N1, yanayotawanyika kwa kasi kitaifa na kimataifa, yana matatizo kuyadhibiti mapema; kunahitajika ushirikiano wa kiwango cha juu kabisa miongfoni mwa sekta zote za afya za Mataifa Wanachama. Kadhia hjii huchukua muda, kwa sababu, kwanza, ni lazima kufanyike utafiti wa kiini cha mripuko na halafu kuandaa tiba na chanjo inayofaa kutumiwa kuyadhibiti maradhi haya kwa mafanikio. Janga la maradhi yanayotawanyika kimataifa kwa kasi lina hatari ya kuambukiza umma wa kimataifa kwa haraka sana, kwa sababu ya ukosefu wa kinga, ndio maana watu huwa na wasiwasi juu ya usalama wa afya ya jamii panapozuka maradhi ya vimelea vipya kama vile vya homa ya mafua ya H1N1.