Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna Mkuu juu ya wahamiaji azuru Pakistan kutathminia hali ya waathirika mapigano

Kamishna Mkuu juu ya wahamiaji azuru Pakistan kutathminia hali ya waathirika mapigano

António Guterres, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Alkhamisi alianza ziara rasmi ya siku tatu katika Pakistan, kufanya tathmini ya mahitaji ya dharura ya kihali ya raia 800,000 waliong\'olewa makazi, kutokana na mapigano makali yalioshtadi karibuni baina ya vikosi vya Serikali na wapambanaji wapinzani, kwenye eneo la kaskazini-magharibi.

Ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuchangisha haraka msaada wa fedha zinazotakikana kuokoa maisha ya umma waathirika. Alikumbusha kwamba Pakistan inawajibika kusaidiwa kidharura na jamii ya kimataifa, kwa sababu katika miaka ya nyuma ilionyesha ukarimu mkubwa kuhudumia kihali mamilioni ya wahamiaji wa kutoka Afghanistan, waliokuwepo nchini humo kwa muda mrefu. UNHCR imeripoti mpaka sasa idadi ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) waliosajiliwa kuhama makwao, kufuatia mfumko wa mapigano kwenye Jimbo la Mpakani la Kaskazini-Magharibi (NWFP) imefikia watu 987,000. Lakini UNHCR inasema fungu kubwa la wahamiaji hawa, waliosajiliwa na serikali Pakistan, na kusaidiwa na UNHCR, huishi kwenye majumba ya jamaa zao au marafiki, na wengine wameamua kufanya makazi ya muda kwenye viwanja badala ya kwenda kwenye kambi za UM. Sehemu ndogo ya wahamiaji, chini ya watu 80,000 ndio walioamua kusihi kwenye makazi ya muda yanayosimamiwa na UNHCR.