Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Uamuzi rasmi wa Serikali ya Cote d’Ivoire kufanyisha uchaguzi wa raisi katika tarehe 29 Novemba 2009, umepokolewa kwa matumaini ya kutia moyo na KM Ban Ki-moon, hususan baada ya serikali kukubali kutekeleza mapendekezo ya Kamisheni Huru ya Uchaguzi. Aliyahimiza makundi yote husika kuihishimu tarehe hiyo na kushirikiana kipamoja kuyakamilisha majukumu yaliosalia yanayoambatana na shughuli za uchaguzi. KM aliwahakikishia raia wa Cote d’Ivoire kwamba UM utaendelea kusaidia kwenye shughuli zote muhimu za kutayarisha uchaguzi, na pia kuhakikisha uchaguzi utafanyika kwa utaratibu ulio huru, wa haki na unaoaminika, na kwa kupitia Ofisi ya Mjumbe wa KM kwa Cote d’Ivoire.

Francis Deng, Mshauri Maalumu wa KM juu ya Uzuiaji Mauaji ya Halaiki ametoa taarifa maalumu kuhusu mzozo uliopamba Sri Lanka katika wiki za karibuni. Kwenye taarifa aliyakumbusha makundi yote mawili yanayohusika na mapigano kuhishimu haki za binadamu, na kutekeleza majukumu yao kama ilivyoidhinishwa na kanuni za kiutu za kimataifa, hasa katika kuwapatia raia walionaswa kwenye mapigano hifadhi kinga dhidi ya mauaji ya kihorera. Aliongeza kusema kikawaida ni watoto wa kike na wanawake watu wazima wanaoathirika kupita kiasi kwenye mazingira ya mapigano, na kwa hivyo aliitaka Serikali iwatekelezee raia hawa wajibu wa kisheria kwa kuwapatia ulinzi bora na hifadhi imara dhidi ya mapigano. Alikumbusha, watu binafsi wanaweza kushtakiwa baadaye na mahakama za kimataifa kushiriki kwenye makosa ya jinai ya vita na makosa mengineyo yanayoambatana na migogoro pindi wanakosa kutekeleza majukumu yao. Mshauri Maalumu wa KM pia kwenye risala yake alitilia mkazo ya kuwa Serikali ya Sri Lanka inawajibika kuwapatia watumishi wa UM waliopo nchini pamoja na wale wanaowakilisha mashirika mengine ya kimataifa yanayohudumia misaada ya kiutu, uhuru kamili wa kuwafikia raia muhitaji pamoja na raia waliopo vizuizini na kwenye vituo vya kusajiliwa, ikijumlisha pia raia waliopo kwenye kambi zote za wahamiaji wa ndani, ili kuhakikisha wanapatiwa mahitaji yao ya kiutu bila ya matatizo. Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) sasa hivi limeanzisha ugawaji vyakula vilivyopikwa tayari kwa maelfu ya wahamiaji waliomiminikia vituo vya ukaguzi kutokea maeneo ya mapigano. Kadhalika Shirika la UNICEF linachangisha kwenye juhudi za kimataifa za kuhudumia maji safi ya kunywa na ya kupikia kwa raia waliong'olewa makazi. Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo linafadhilia vituo kadha wa kadha vya afya madawa na vifaa vya upasuaji. Kuhusu taarifa nyengine juu ya mgogoro wa Sri Lanka, Ofisi ya Kamishna Mkuu juu ya Haki za Binadamu imetoa pendekezo linalotaka kuundwe tume maalumu ya uchunguzi juu ya namna vita vilivyoongozwa nchini humo na kama vilifuata kanuni za mapigano au la. Tume pia inatarajiwa kuthibitisha idadi halisi ya raia waliouawa.

Ijumaa (15/05/2009) asubuhi Baraza la Usalama limepitisha taarifa rasmi ya raisi, kwa waandishi habari, juu ya Usomali. Ndani ya taarifa hii Baraza la Usalama limehimiza jamii ya kimataifa kuunga mkono, kwa ukamilifu, Serekali ya Mpito ya Usomali na kuiwezesha kuimarisha Vikosi vya Usalama vya Taifa pamoja na Polisi. Vile vile taarifa ilisisitiza Baraza linaunga mkono kidhati mchango wa vikosi vya ulinzi amani katika Usomali vya Umoja wa Afrika (AMISOM), na kulaani uhasama wowote dhidi yao. Baraza la Usalama limeeleza kuwa na wahka mkubwa juu ya kuharibika zaidi kwa hali ya kiutu nchini baada ya mapigano kufufuka tena Usomali, na inawataka makundi husika kutekeleza majukumu yao chini ya sheria za kiutu za kimataifa, hususan ile kanuni ya kuhishimu usalama wa raia na usalama wa wahudumia misaada ya kiutu pamoja na wale watumishi wa AMISOM.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba Maombi ya Jumla yaliotangazwa Novemba 2008 kwa Mataifa Wanachama kuchangisha msaada wa fedha zinazohitajika kuhudumia maafa ya dharura katika nchi saba za Afrika Mashariki na Kati, yamemudu kuchangisha asilimia 27 tu ya maombi hayo, licha ya kuwa maeneo haya ndio yenye kuhitaji zaidi misaada ya kiutu duniani. Nchi zinazoambatana na kadhia hii zinajumlisha Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Usomali, Sudan na Uganda. Msaada halisi wa asilimia 27 ya maombi uliofadhiliwa OCHA ulipokelewa mnamo tarehe mosi Aprili 2009.

Michel Sidibé, aliye Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) ametangaza taarifa maalumu inayozitaka serikali za kimataifa kuondosha tabia ya kufedhehi na kubagua wasenge/makhanithi na mabasha, pamoja na wasagaji na wale watu waliobadilisha jinsiya. Taarifa hii ilitolewa Ijumaa ya leo kabla ya walimwengu kuiadhimisha Ijumapili (17 Mei 2009) ‘Siku ya Kimataifa Dhidi ya Woga wa Wasenge na Mabasha'. Kadhalika Sidibé alipendekeza serikali ziandae mazingira ya kisheria na kijamii yatakayohakikisha haki za binadamu zitahishimiwa na kuwawezesha watu muhitaji kusaidiwa kupata uangalizi, matibabu na kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI.