Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya msemaji wa KM imetangaza kuteuliwa kwa Franz Baumann wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, kuongoza Idara ya Usimamizi wa Mikutano pamoja na Shughuli za Baraza Kuu (DGACM).

KM ameripoti kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa mpinzani wa Myanmar, Daw Aung San Suu Kyi ambaye ameripotiwa kuhamishwa kutoka kifungo cha nyumba na kupelekwa kwenye Gereza la Insein kukabili kesi ya jinai. KM anaamini Daw Aung San Suu Kyi ni mshiriki muhimu sana kwenye majadiliano ya Myanmar juu ya upatanishi wa taifa. Alirudia nasaha aliotangaza kabla kwamba Daw Aung San Suu Kyi, na wale wote wenye uwezo wa kuchangia amani ya kudumu nchini mwao, ni lazima wawe na uhuru wa kuweza kuyatekeleza hayo, hali ambayo itahakikisha kidhati kwamba mfumo wa siasa ndani ya nchi ni wa kuaminika.

Vijay Nambiar, Mkuu wa Baraza la Ofisi ya KM, amepelekwa Sri Lanka na ujumbe maalumu wa KM, kwa makusudio ya kujaribu kusuluhisha matatizo ya kiutu yaliopamba kieneo kwa sasa hivi. Wajumbe wa Baraza la Usalama wameripoti kuwa wanaunga mkono juhudi za binafsi za KM za kusuluhisha mzozo uliopamba Sri Lanka. Baraza la Usalama limeisihi Serikali ya Sri Lanka kushirikiana, kwa ukamilifu, na Mjumbe wa KM, ili kutatua mgogoro hatari wa kiutu uliopamba nchini.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limelaani mashambulio maututi, dhidi ya raia na wanajeshi wa taifa, yaliotukia majuzi kaskazini-mashariki katika jimbo la Walikale. MONUC imeanzisha upelelezi juu ya tukio hili ambalo lilisababisha vifo vya watu 35 na kuwalazimisha wakazi 15,000 kuhama makwao. Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, Alan Doss, alisema mashambulio haya humaanisha jeshi la taifa nchini ni lazima liimarishwe, kutekeleza kama inavyotakikana huduma za kulinda vyema raia.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah ametoa taarifa yenye kuwalaumu watu wenye siasa kali,wanaodaiwa kuhujumu mji wa Mogadishu, kuhusika moja kwa moja na usumbufu na mateso wanaoshuhudia makumi elfu ya raia wa Usomali. Alisisitiza mapigano ya karibuni yalisababisha vifo na watu wingi kung'olewa makazi, hususan wale ambao walirejea Mogadishu karibuni kwa matumaini ya kuanzisha maisha mapya kwa dhana hali imetulia. Mjumbe wa KM alisema umma muhitaji wa Usomali unahitajia misaada ya dharura kutoka wahisani wa kimataifa ili kunusuru maisha.

Tume maalumu ya Baraza la Usalama imeondoka New York alsiri kuelekea Afrika ambapo watazuru mataifa ya Ethiopia, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) na Liberia. Mabalozi wa Ufaransa, Uganda, Uingereza na Marekani wataongoza tume katika sehemu tofauti za safari.

Shirika la Ulinzi Amani katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT) limeripotiwa wiki hii kupokea wanajeshi wapya 131 wa Ghana watakaosambazwa kwenye jimbo la Farchana mashariki ndani ya Chad. Wanajeshi hawa watajiunga na wenziwao 71 wengine waliowasili nchini mnamo siku za nyuma. Inatarajiwa vikosi vya MINURCAT vitakapokamilishwa, kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Usalama kwa kujumlisha askari 5,200, wanajeshi 800 kati ya hao watawakilisha taifa la Ghana. Lengo la MINURCAT kieneo ni kuwapatia hifadhi watu waliomo hatarini, hasa wale wahamiaji waliotokea eneo jirani la Darfur pamoja na raia wa Chad waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano. Kadhalika vikosi vya MINURCAT vitatumiwa kuhudumia ugawaji wa misaada ya kiutu kwa wahitaji na kuhakikisha pia watumishi wa mashirika yanayohudumia misaada ya kihali wana uhuru wa kuendeleza shughuli zao bila kusumbuliwa au uchokozi.

Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina kwa Mashariki ya Karibu (UNRWA) wiki hii litaanza taadhima mbalimbali za kutimiza miaka 60 tangu lilipoanzishwa. Kwa mujibu wa UNRWA kumbukumbu hizi zitazitafanyika katika sehemu kadha wa kadha za dunia, ikijumlisha New York, Vienna, Brussels na Beirut. Taadhima rasmi zitaanzishwa Ijumaa na Mkurugenzi Mkuu wa UNRWA, Karen AbuZayd kwenye mji wa WaFalastina wa Ramallah. Wakati huo huo Papa Benedict XVI Ijumatano alizuru kambi ya UNRWA ya wahamiaji wa KiFalastina karibu na Bethlehem, ambapo alitoa mchango wa uro 50,000 zitakazotumiwa kusaidia kujenga madarasa matatu mapya ya wanafunzi wa kiume wa KiFalastina.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti Alkhamisi (14 Mei 2009) kwamba jumla ya wagonjwa 6,500 walisajiliwa rasmi kuambukizwa na vimelea vya homa ya mafua ya A(H1N1) katika nchi 33. Ijapokuwa idadi ya wagonjwa walioambukizwa na maradhi imeongezeka, WHO imenasihi umma wa kimataifa usijisumbue kwa "kujitia wasiwasi uliopita kiasi" kukhofu maradhi, kwa sababu taasisi ya afya ya UM haijapwelewa katu kwenye uchunguzi wake, uanofuatiliwa kwa ukaribu zaidi, kuhusu hali ya maambukizi ya homa ya mafua ya H1N1 ulimwenguni, maradhi ambayo hayathibitisha makali ya kushtusha. WHO ilitilia mkazo kwenye taarifa yake kwamba maambukizi ya homa yamedhihirika kwa wingi katika nchi mbili tu: nazo ni Marekani na Mexico. Ripoti ya WHO iliongeza kusema kwamba hali ikibadilika au ikibainisha dalili za kutisha, walimwengu wataarifiwa, halan, juu ya taratibu za kuchukuliwa kujikinga dhidi ya mripuko hatari wa maradhi