Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti katika milango ya saa 4 asubuhi, leo Ijumatano, waangalizi wa kijeshi walishuhudia ndege za Serikali ya Sudan zikishambulia kwa mabomu maeneo ya kaskazini ya Um Baru, mji wa Darfur Kaskazini ambao katika siku za karibuni ulifunikwa na mapigano makali. Makundi ya wafuasi wa Minni Minawi wa SLA walipambana na wafuasi wa kundi la JEM kwenye eneo liliopo jirani na mji wa Um Baru. Ijumatatu iliopita waangalizi wa vikosi vya amani vya UNAMID walishuhudia tena mashambulio ya anga ya ndege za Serikali ya Sudan kwenye eneo hilo.

B. Lynn Pascoe, Naibu KM kwa Masuala ya Kisiasa aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama, kwenye mkutano wa hadhara kuzingatia Usomali, kwamba mkusanyiko wao unafanyika katika kipindi muhimu kabisa kuhusu maendeleo ya amani ya kwenye taifa hili la Pembe ya Afrika. Alisema jamii ya kimataifa ina matumaini ya kutia moyo, baada ya kubainika umma wa Usomali sasa hivi una fursa kubwa ya kukomesha mateso, na kuanzisha safari ndefu ya kujenga amani itakayodumu, na kurudisha utulivu kwa wakati ujao. Pascoe alisema mfumko wa fujo za karibuni umedhihirisha wapinzani wameghadhibika na sera ya serikali, ya kutaka kujumuisha umma kwenye jitihadi za kurudisha utulivu na amani ya nchi. Naibu KM juu ya Operesheni za Amani za UM Ulimwenguni, Alain Le Roy, yeye kwa upande wake aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama ya kuwa UM upo tayari kujiunga kwenye huduma za kurudisha amani Usomali, pindi taratibu za viwango vitatu zitatekelezwa kwa kiawamu. Le Roy alisisitiza kwamba kwa kulingana na changanuzi za KM, kwa sababu ya hali ya hatari kubwa na kigeugeu iliojiri Usomali, kwa sasa, haamini itawezekana kwa UM kuanzisha operesheni mpya za kulinda amani nchini humo, maana katika hali ya mazingira ya kigeugeu na wasiwasi, kama ilivyodhihiri hivi sasa, operesheni za amani za UM hazitokuwa na matumaini ya kufanikiwa.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kushtadi kwa mapigano, kwenye eneo la mgogoro katika Sri Lanka, baina ya vikosi vya serikali na wapinzani, hali iliosababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi kwa raia. Kadhalika, OCHA imeeleza kuarifiwa na Serikali ya Sri Lanka kwamba itaanza kutoa kadi za utambulisho kwa wahamiaji raia wa ndani (IDPs), wakimaliza kusajiliwa rasmi na wenye mamlaka, vitambulisho ambavyo vitawaruhusu wao kusafiri nje ya kambi za makazi ya muda kutafuta ajira, na kununua vyakula na mahitaji mengine ya maisha. Wahamiaji wa IDPs 20,000 wameshasajiliwa hivi sasa, kadhia ambayo bado inaendelea kushughulikiwa na serikali. Usimamizi wa kambi za wahamiaji raia sasa hivi unaongozwa na wanajeshi wa Sri Lanka, licha ya kuwa UM unaendelea kusisitiza wanaowajibika kushughulikia kambi hizi kihakika ni raia. Serikali imetakiwa izipatia kambi za wahamiaji wa IDPs ulinzi wa mapolisi, hasa askari wa kike, na hususan wale polisi wa kutoka jamii ya WaSriLanka wenye asili ya Ki-Tamili.

Leo asubuhi KM alihutubia ufunguzi wa kikao cha 17 cha Hadhi ya Juu cha Kamisheni juu ya Maendeleo Yanayosarifika kilichofanyika hapa Makao Makuu. Alisema kwenye risala yake kwamba rai ya kuwa na maendeleo ya kusarifika ni wazo lilioanzishwa miaka 20 iliopita na Umoja wa Mataifa, wazo ambalo uhalali wake utaendelea kutambuliwa kimataifa kwa muda mrefu ujao. Kwa mujibu wa KM rai ya kuwa na sera inayofungamanisha, kwa ujumla, huduma zote za maendeleo ni mwelekeo wenye uwezo hakika wa kukabiliana kidhati na matatizo yanayohusu maendeleo, kama athari za mabadiliko ya hali ya hewa, mizozo ya chkula kwenye soko la kimataifa na yale matatizo yanayochochewa na bei ya kigeugeu ya nishati. Alisisitiza KM mwelekeo kama huu ndio wenye suluhu inayodumu katika kukabiliana, kwa mafanikio, na matatizo yanayoletwa na mzoroto wa uchumi wa kimataifa na mizozo ya fedha duniani.

Kamisheni ya Mamlaka ya Mipaka ya Uketo wa Bahari imeripoti kwamba kwenye saa sita za usiku Ijumanne (12 Mei 2009) ilikabidhiwa madai 50 kuhusu mamlaka ya maeneo ya bahari kutoka mataifa ya mwambao yalioridhia Mkataba wa UM juu ya Sheria ya Bahari. Siku hiyo ilikubaliwa kuwa ni siku ya mwisho kwa wadau husika na Mkataba, kuwasilisha madai yao kuhusu maeneo ya mamlaka yanayoambatana na uketo wa bahari, nje ya eneo linalotambuliwa kama "eneo la shughuli za uchumi pekee" kama ilivyokubaliwa na wajumbe wa kimataifa mwezi Mei 1999. Chini ya kanuni za Mkataba, mataifa ya mwambao yana haki ya kudai mamlaka ya uketo wa bahari, nje ya maili 12 ya mipaka yao ya baharini na pia kudai mipaka ya maili 200 ya eneo la kuhudumia uchumi pekee.