Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia elfu ya raia wa kaskazini-magharibi katika Pakistan wahajiri makazi baada kuzuka mapigano

Mamia elfu ya raia wa kaskazini-magharibi katika Pakistan wahajiri makazi baada kuzuka mapigano

UM umepokea taarifa zilizothibitisha kushtadi kwa mapigano baina ya majeshi ya serikali na wapinzani kwenye bonde la Swat, liliopo kwenye Jimbo la Mpakani Kaskazini-Magharibi katika Pakistan, yaani katika Jimbo NWFP.

 Ripoti zinasema zaidi ya watu 360,000 wameng'olewa makwao na kuhajiri makazi kuepukana na mapigano yaliofumka karibu wiki moja iliopita. Maofisa wa UM wanahadharisha idadi ya wahajiri hawa huenda ikaongezeka kama haijadhibitiwa mapema. Mwandishi habari wa Redio ya UM, Don Bobb, alipata fursa ya kuhojiana na Arianne Rummary, Msemaji wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) katika Pakistan, kuhusu mchango wa UM katika kuhudumia kihali umma huo ulioathirika na mapigano katika Jimbo la Mpakani:

"UM kwa ujumla, na hasa UNHCR, zimeanzisha kambi maalumu za kuhudumia waathirika wa mapigano na vurugu, makazi ya muda, kwenye yale maeneo salama yaliopo karibu na sehemu za mapigano. Tumewapatia umma huo mahema, maji safi na vifaa vya afya. Kadhalika, kwenye vituo vya UM tunasaidia kuwapatia waathirika hawa mablanketi, majora ya plastiki, madumu ya jerikeni pamoja na vifaa vya kupikia. Kusema kweli, tunaihudumia idadi ndogo ya watu waliong'olewa makazi na mapigano .. kwa sababu mila za maeneo haya haziruhusu watu kukaa kambini, na wahamiaji husika hufanya kila wawezalo kukwepa makazi kama haya na badala yake hujaribu kutafuta suluhu mbadala, kama vile kukaa na jamaa zao au watu wa kabila yao. Kwa hivyo, vifaa hivi vya kumudu maisha ya muda tunawajibika pia kuwafarajia wale wahamiaji waliopo nje ya kambi zinazosimamiwa na UM."