Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekaji mipaka Abyei wazingatiwa na mahakama ya PCA

Uwekaji mipaka Abyei wazingatiwa na mahakama ya PCA

Mnamo Alkhamisi,07 Mei (2009) Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi, au Mahakama ya PCA, iliopo kwenye mji wa Hague, Uholanzi, ilimaliza kusikiliza hoja za watetezi wanaowakilisha makundi mawili yanayohusika na uwekaji mipaka rasmi ya ule mji wa Abyei, uliotawanyika kwenye eneo la kaskazini na kusini katika Sudan.

Kuanzia wiki tatu nyuma, Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA) ilianzisha mahojiano ya kuwekea mipaka mipya mji wa Abyei, suala ambalo limezusha mvutano mkubwa kati yale makundi mawili yalioshiriki kwenye mapigano ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe katika Sudan. Makundi haya mawili yalijumlisha kundi la NCP, linalowakilisha serikali ya kaskazini, na kundi la SPLM, ambalo zamani lilikuwa likiongoza jeshi la mgambo la Sudan kusini. Moja ya sababu ilizoyahamasisha makundi mawili haya kukubali kutia sahihi Mapatano ya Jumla ya Amani katika 2005, ilikuwa ni makubaliano ya kuitaka mahakama ya kimataifa kusuluhisha tatizo la mipaka ya mji wa Abyei, na waliahidi kuyatekeleza maamuzi ya mahakama kama inavyotakiwa kisheria.

Kwenye taarifa iliotangazwa baada ya kumalizika mahojiano ya mdomo, na ya maandishi kwenye Mahakama ya PCA, kwenye juhudi za kuleta suluhu ya mwisho kuhusu mzozo wa Abyei, KM alinakiliwa akisema ameridhika na tukio hili. Wakati huo huo aliyahimiza makundi yanayohusika na suala la Abyei yashirikiane, kidhati, kwenye mazungumzo yatakayohakikisha mvutano wao utasuluhishwa kwa amani, na kwa ridhaa ya wote. Kwa mujibu wa KM makundi ya NCP na SPLM yamesisitiza kuwa yatatii, na kutekeleza bila ya mwanya, uamuzi wa Mahakama ya PCA.

Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA), ambayo huungwa mkono na UM, ni shirika la serikali mbalimbali zinazowakilisha wajumbe kutoka mataifa wanachama zaidi ya mia moja. Mahakama hii lilibuniwa rasmi mwaka 1899, kwa makusudio ya kusaidia kusuluhisha mizozo baina ya mataifa, kwa kutumia sheria ya kimataifa ya binafsi na sheria ya umma, kwa kushughulikia mizozo inayobadilika mara kwa mara, katika jamii nzima ya kimataifa. Hivi sasa, Mahakama ya PCA hushughulikia kesi zinazohusu mchanganyiko wa matatizo kadha wa kadha, yale yanayosumbua mataifa, vitengo vya kitaifa na pia matatizo ya mashirika yanayohusu serikali mbalimbali na vile vile makundi ya binafsi. Makao Makuu ya Mahakama, yanaongozwa na KM wake maalumu, na ndipo kunapofanyika usajili wa huduma kamili zinazotumiwa kuipatia mahakama uwezo wa kiutawala na misaada ya sheria kwa kamisheni na tume za usuluhish