UNICEF imehadharisha, siasa za kigeugeu na vurugu vyahatarisha njaa kwa watoto wa Pembe ya Afrika

UNICEF imehadharisha, siasa za kigeugeu na vurugu vyahatarisha njaa kwa watoto wa Pembe ya Afrika

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limehadharisha ya kuwa mchanganyiko wa matatizo sugu ya chakula na hali iliopamba ya kigeugeu cha kisiasa kieneo, yanahatarisha ustawi na maisha ya mamilioni ya jamii ya watoto wanaoishi kwenye eneo la Pembe ya Afrika.

Miranda Eeles, msemaji wa UNICEF aliwapatia waandishi habari Geneva asubuhi maelezo zaidi juu ya msiba huo kama ifuatavyo:

"Tayari watu milioni 19.8, ikijumlisha watoto wachanga milioni nne chini ya umri wa miaka mitano, wanahitajia sasa hivi kufarajiwa misaada ya dharura ya kunusuru maisha. Huu ni muongezeko mkubwa wa jumla ya watu wanaohitajia misaada ya dharura ya kihali kutoka mashirika ya kimataifa, tukilinganisha na takwimu za mwezi Septemba 2008, ambapo watu milioni 14 walihitajia kuhudumiwa kihali na wahisani wa kimataifa. Mnamo miezi michache iliopita UNICEF iliripoti kuongezeka kwa jumla ya watoto wadogo waliokuwa wakiugua utapiamlo mkali kwenye eneo. Takwimu zilizokusanywa na wataalamu wa lishe, hasa katika vile vituo vya kuhudumia chakula vya UM, zimethibitisha kihakika kwamba idadi ya watoto wachanga wanaogua utapiamlo hatari imeongezeka kwa kima kikubwa, hali ambayo inakhofiwa kama haijadhibitiwa mapema huenda ikasababisha janga kuu la vifo."