Hali ya usalama Chad Mashariki inaripotiwa kuharibika
UM umeripoti mapigano yaliozuka mapema wiki hii baina ya vikosi vya serikali na waasi, katika Chad Mashariki, yameathiri shughuli za kuhudumia kihali wahamiaji wa Sudan 250,000 pamoja na wahajiri wa ndani ya nchi 166,000.
UM umeyasihi makundi yanayohasimiana huko kuhishimu sheria za kiutu za kimataifa za kuhifadhi raia, hususan watoto wadogo na wanawake, dhidi ya athari za mapigano. Licha ya kufumka kwa vurugu hili, karibu na kambi za wahamiaji, ziliopo katika eneo la Koukou Angarana, Chad Mashariki, msemaji wa UNHCR, Ron Redmond leo asubuhi aliwaarifu waandishi habari wa kimataifa Geneva ya kwamba operesheni za kunusuru maisha, za UM bado zinaendelezwa kwenye eneo la mapigano. Kadhalika UNHCR imeripoti kuzuka mapigano mapya Alkhamisi kwenye sehemu ya Am Dam, kilomita 100 kutoka Abeche, mji mkuu wa Chad mashariki. Mnamo kati ya wiki, kwa sababu ya mazingira ya mtafaruku kieneo UNHCR ililazimika kuwahamisha watumishi 18 - kwa sababu ya usalama - kutoka sehemu ya Koukou na kuwapeleka kwenye eneo la Goz Beida, liliopo kilomita 50, mbali na vurugu. Halkadhalika, asubuhi kwenye ukumbi wa Baraza la Usalama kulifanyika kikao cha hadhara kuzingatia hali katika Chad. Baada ya hapo kulifanyika kikao cha faragha, cha mashauriano miongoni mwa wajumbe wa Baraza kuzingatia hali halisi katika Chad, na katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na pia kusailia usalama wa eneo, kijumla.