Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa ya WHO juu ya Homa ya H1N1

Taarifa ya WHO juu ya Homa ya H1N1

Tunaanza na ripoti ya takwimu zilizotangazwa Alkhamisi na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya maambukizi ya homa ya mafua ya A(H1N1) katika ulimwengu.

 Kuanzia saa 06:00 za majira ya GMT jumla ya nchi 23 zimeripoti rasmi kwa WHO kuwa zimegundua wagonjwa waliopatwa na virusi vya homa ya mafua ya H1N1 kwenye maeneo yao. Jumla ya wagonjwa walioambukizwa na homa ya H1N1, kwa sasa, kwenye nchi hizi ni 2099.  Mexico iliripoti kuwa na wagonjwa 1112 wa homa ya mafua ya H1N1, na kusajili vifo 42 kutoka idadi hiyo. Marekani imeripoti wagonjwa 642 walisajiliwa kuambukizwa na homa ya H1N1, na wagonjwa wawili walifariki maradhi. Mataifa yafuatayo nayo pia yameripoti kugundua wagonjwa walioambukizwa na virusi vya homa ya mafua ya H1N1, lakini hakuna aliyeripoti kifo - Austria (1); Kanada (201), Hong Kong, Uchina (1), Colombia (1), Costa Rica (1) Denmark (1), El Salvador (2), Ufaransa (5), Ujerumani (9), Guatemala (1), Ireland (1), Israel (4), Utaliana (5), Uholanzi (1), New Zealand (5), Ureno (1), Jamhuri ya Korea (Korea ya Kusini) (2), Uspeni (73), Uswiss (1) na Uingereza (28).