Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumanne Baraza la Usalama lilipitisha Taarifa ya Raisi ilioleza jamii ya kimataifa kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mtindo uliozuka karibuni katika baadhi ya nchi za KiAfrika, ambapo mageuzi ya serikali yalifanyika yasiolingana na mfumo wa kikatiba. Risala ya Raisi wa Baraza la Usalama ilitia mkazo umuhimu wa kurudisha haraka mfumo wa kikatiba katika sehemu hizo za Afrika, ili kuwasilisha mabadiliko ya serikali kwa taratibu za amani, ikijumlisha pia zile kadhia za kufanyisha chaguzi za kuaminika, zenye uwazi na za haki.

KM Ban Ki-moon aliripotiwa na msemaji wa UM kwamba alikutana asubuhi kwenye Makao Makuu, na Shimon Peres, Raisi wa Israel na walijadiliana masuala matatu: ripoti ya Bodi la Uchunguzi juu ya Tarafa ya Ghaza; suala la kijiji cha Ghajar, Lebanon na pia Mkutano wa Mapitio ya Azimio la Durban dhidi ya Ubaguzi. Kwenye mazungumzo yao haya KM alimwambia Raisi Peres kuwa anaunga mkono ombi la Jaji Richard Goldstone anayeongoza tume ya uchunguzi ya Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu [iliodhaminiwa jukumu la kuendeleza ukaguzi wa masuala yanayofungamana na mapigano yaliotukia Ghaza karibuni]. KM aliihimiza Israel ishirikiane na tume hii ya uchunguzi ya UM.

Wiki hii kwenye mji wa Nicosia, Cyprus kumefanyika Mkutano wa Kimataifa juu ya Amani ya Falastina-Israel, ulioongozwa na Kamati ya UM ya Kutekeleza Haki Zisiofutika za Umma wa KiFalastina. Kwenye risala alioituma mkutanoni, KM alihimiza kufufuliwa tena mashauriano ya amani, na kuyataka yazingatie, kwa kina, masuala yote ya kimsingi, na bila ya mwanya wa aina yoyote. Risala ya KM ilisomwa mbele ya wajumbe wa kimataifa na Taye-Brook Zerihoun, Mjumbe Maalumu wa UM kwa Cyprus.

Mahakama ya UM juu ya Rwanda, iliopo Arusha, Tanzania imeanza kusikiliza kesi ya Dominique Ntawukulilyayo, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Butare, Rwanda na ambaye alituhumiwa mashtaka matatu ya mauaji ya halaiki, ikijumlisha lile kosa la kushawishi watu kuendeleza mauaji ya kihorera. Waendesha mashtaka wamedai Ntawukulilyayo alishindwa kuzuia mauaji ya umma kwenye yale maeneo yaliokuwa chini ya madaraka yake, na inaripotiwa pia kwamba katika baadhi ya matukio hayo alikuwa kama manjo aliyechochea na kushawishi watu kufanya mauaji ya halaiki. Mtuhumiwa huyu alishikwa Ufaransa katika 2007, na mwaka uliopita alipelekwa Arusha kwenye Mahakama ya ICTR kukabili kesi. Ntawukulilyayo amekana makosa yote dhidi yake.

Gregory B. Starr, raia wa Marekani ameteuliwa hii leo na KM kuwa KM Mdogo wa Masuala ya Ulinzi na Usalama katika UM, baada ya David Veness, aliyemtangulia kwenye cheo hicho, kukamilisha mkataba wake na UM. Kwa mujibu wa ripoti za UM Starr ana uzoefu mkubwa katika usimamizi wa operesheni za usalama duniani unaohusika na taasisi za kiraia, na alihusika pia kwenye maandalizi ya sera za ulinzi kwa kutayarisha vigezo vya kuendesha shughuli za kazi kwa usalama madhubuti. Uamuzi wa KM kumteua Starr kuongoza Idara ya Usalama na Ulinzi katika UM umechukuliwa katika nyakati ambapo UM hukabiliwa na mazingira ya vitisho vya aina kwa aina ulimwenguni, na kuambatana na uzoefu alionao inaaminika Starr ataweza kuanza kuitumikia UM mapema zaidi. Tangu 1980 Starr alitumikia Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya Marekani. Hivi sasa Starr ni Mkurugenzi wa Huduma za Usalama wa Kidiplomasiya na pia Naibu Waziri wa Kitengo cha Ulinzi wa Kidiplomasiya katika Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani. Starr aliwahi kuitumikia Idara hiyo katika nchi za Israel, Senegal, Tunisia na katika taifa liliojulikana zamani kama Zaire.

Shirika la UM juu ya Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeripoti kusita kutumia yale majina ya vimbunga ya Gustav, Ike, Paloma na Alma, majina ambayo yangelitumiwa tena 2014, kwa kuambatana na kanuni za WMO. Moja ya sababu iliotolewa ni kwamba vimbunga vya 2008 vilivyopewa majina haya vilisababisha vifo na uharibifu mkubwa katika yale maeneo yaliovamiwa na matofani. Majina yatakayotumiwa 2014 na WMO kwa vimbunga vitakavyotukia wakati huo yatakuwa Gonzalo (badala ya Gustav), Isaias (kuwakilisha Ike), Paulette (kutumiwa badala ya Paloma) na pia Amanda (badala ya Alma).