Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asubuhi ya leo, kwa kupitia njia ya video aliwaambia wajumbe wa kimataifa waliohudhuria kikao kisio rasmi cha Baraza Kuu, kilichofanyika asubuhi kwenye Makao Makuu ya kuwa taasisi yao imepokea ripoti zilizothibitisha jumla ya wagonjwa 1,003 kutoka nchi 20 ziliopo katika mabara manne, waligundulikana kuambukizwa na homa ya mafua ya H1N1.

Kadhalika, alisema WHO imeshatuma sasa hivi dozi milioni 3 za tiba ya homa ya mafua katika nchi 70, asilimia kubwa yao ikiwa zile nchi masikini.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limetoa onyo maalumu kwa wenye madaraka, pamoja na wakulima, katika Kanada linalowataka wachunguze kwa ukaribu zaidi afya ya wanyama wanaofugwa, hasa nguruwe, ili kuhakikisha hawajaambukizwa na homa ya mafua ya H1N1. Onyo hili lilitolewa baada ya nguruwe kugundulikana kuambukizwa na vimelea vya H1N1 kutoka mwanadamu.

KM ameyakaribisha Maafikiano yaliotiwa sahihi mnamo tarehe 03 Mei,  kwenye mji wa Doha, baina ya Serikali za Chad na Sudan, ya kusitisha uhasama kati yao, mwafaka uliosimamiwa na Mataifa ya Qatar na Libya. KM alitumai maendeleo haya ya kutia moyo yatasaidia kuhamasisha makundi husika kupunguza hali ya wasiwasi iliojiri hapo kabla baina ya mataifa haya mawili, na kuandaa mazingira yatakayosaidia kurudisha tena utulivu na amani ya eneo lao.

Kadhalika, KM aliripoti kuingiwa wasiwasi juu ya kuzorota kwa hali ya hatari Bukini, ambapo wapinzani dhidi ya wenye madaraka walishikwa kwa sababu ya mamlaka ya kisiasa, kinyume na sheria na haki za binadamu. Alisema hatua kama hii ndio inayopalilia fujo na kusababisha watu kupoteza maisha. KM aliahidi UM utajihusisha na juhudi zote za kurudisha amani Bukini, na alimkabidhi jukumu hilo Tiébilé Dramé, Mshauri wa Ngazi ya Juu wa UM kuhusu Masuala ya Kisiasa, ambaye alipata fursa ya kushauriana na wawakilishi wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya SADC na pia na wadau wengine kuhusu taratibu za kutumiwa kwa pamoja na jumuiya ya kimataifa, kwa pamoja, kurahisisha utatuzi wa mgogoro husika katika Bukini.

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti wapiganaji 44, wa kutoka makundi ya mgambo yaliojitenga, wametia sahihi Azimio la Kuahidi Kutekeleza Mapatano ya Amani ya Darfur, baada ya kujiunga rasmi na Jeshi la Taifa, na kufuatia mafunzo ya miezi sita ya kijeshi.

Kwenye chumba cha kusikiliza kesi, cha Mahakama Maalum juu ya Jinai ya Vita katika Sierra Leone, kumetolewa ilani ya kukataa kwa ukamilifu lile ombi la timu ya mawakili wa utetezi, la kumwachia huru kutoka kizuizini, aliyekuwa Raisi wa Liberia, Charlesa Taylor. Mahakama ilisisitiza Taylor antarajiwa kujibu, binafsi, mashitaka yote 11 aliyotuhumiwa nayo ya kushiriki kwenye jinai ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopamba Sierra Leone miaka ya nyuma.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kuwa limefanikiwa kuwatoa watoto 23 kutoka safu za wapiganaji wa majeshi ya mgambo Kivu Kaskazini, mnamo siku za karibuni.