Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

John Holmes, KM juu ya Masuala ya Kiutu na Misaada ya Dharura ameshtumu, kwa kauli kali, mashambulio ya raia yaliofanyika karibuni kwenye jimbo la Kivu Kusini, katika JKK, na kundi la waasi la FDLR.

Alisema waasi wa FDLR wameamua kutumia nguvu na fujo dhidi ya raia kufuatia tangazo la jeshi la taifa la JKK kuwa linajiandaa kuendeleza operesheni mpya za kuwaondosha wapiganaji wa FDLR kutoka yale maeneo wanayoyatumia kuhujumu na kutesa raia Kivu Kusini. Tangu mwanzo wa mwaka wakazi dhaifu karibu 100,000 waling'olewa mastakimu yao na waasi, kwa kutumia vurugu na fujo. Holmes alihadharisha mapigano ya karibuni yanaashiria mamia elfu kadha ya raia yanakabiliwa na hatari ya kuhamishwa tena kutoka makazi yao ya muda. Alisihi makundi yote ya mgambo kuhakikisha yanawapatia raia ulinzi bora na hifadhi ya vibarua, na wakati huo huo kuruhusu wahudumia misaada ya kiutu kuyafikia maeneo waliopo umma huo ili kukidhi mahitaji yao ya kihali.

UM umeripoti idadi ya watu waliouawa Angola kutokana na mafuriko ya karibuni, imefikia watu 60 kwa hivi sasa, na watu 81,000 ziada wamelazimika kuyahama makazi baada ya nyumba 4,000 kuharibiwa na kuangamizwa. Wakati huo huo jumla ya dola milioni 2.3 zimeruhusiwa kutolewa kutoka Mfuko wa UM juu ya Maafa ya Dharura (Mfuko wa CERF) kuwasaidia watu muhitaji. Fedha hizo vile vile zitatumiwa kuzisaidia jamii zilizong'olewa makaazi kupata maji safi ya matumizi pamoja na usafi wa mazingira na pia katika kuhudumia miradi ya afya. Kadhalika, kwenye majimbo ya Namibia ya kaskazini ya kati na kaskazini-mashariki ambapo kuliannguka mvua kali na mafuriko makubwa watu 92 waliuawa huko na raia 54,000 waliripotiwa kung'olewa makazi.